Rais Samia aomboleza kifo cha Naibu Waziri Ole Nasha

NA GODFREY NNKO

Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, William Ole Nasha amefariki dunia Septemba 27, 2021 nyumbani kwake jijini Dodoma.
Kifo Cha Mheshimiwa Ole Nasha kimethibitishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

"Nasikitika kuwajulisha kuwa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji Mhe. William Tate Ole Nasha amefariki dunia Jijini Dodoma. Natoa pole kwa Spika Mhe. Job Ndugai, Wabunge, Familia na Wananchi wa Ngorongoro. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.
Kwa nyakati tofauti wanakijiji wa vijiji vilivyopo Tarafa ya Loliondo katika Jimbo la Ngorongoro wilayani Ngorongoro wamemweleza MWANDISHI DIRAMAKINI kuwa, taarifa za kifo cha Mheshimiwa Ole Nasha ni pigo kubwa kwao.

"Hakika kifo ni fumbo kubwa mno. Taarifa za kifo cha Mheshimiwa Ole Nasha nimezisikia, zimenihuzunisha sana. Mzee wetu alikuwa mzalendo namba moja. Ametufanyia mambo mengi kwa kipindi kifupi akiwa jimboni.

"Miongoni mwa mambo ambayo ameyatekeleza ni pamoja na barabara, umeme na amekuwa mtu mwema sana katika kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiuchumi, kwani kwa upendo wake, wengi tumevuka kiuchumi,"amesema Kijoa mkazi wa Orkuyene.

Wakati huo huo, Meseyi Mejoli amesema kuwa, Mheshimiwa Ole Nasha wakati wa uhai wake alikuwa mtu msikivu na mnyenyekevu, hivyo wamepoteza mtu muhimu katika jimbo lao na Taifa kwa ujumla.

Amesema, tabia ya unyenyekevu na kujishusha kwa makundi yote ya kijamii yalimfanya Mheshimiwa Ole Nasha hata akipigiwa simu bila kujali usiku wa manane kwa ajili ya kupatia ufumbuzi changamoto za wananchi wake. Alikuwa anapokea na kuchukua hatua za haraka.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news