DCI: Uchunguzi umebaini Hamza alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga

MWANZA, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura ameeleza kuwa, uchunguzi uliyofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kwamba Hamza Mohammed alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga.
Hamza aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi jirani na ulipo ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Alhamisi Septemba 2, 2021 jijini Mwanza na waandishi wa habari Wambura amesema, uchunguzi huo ulijikita katika mambo makuu matatu ambayo ni kutaka kutambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma Hamza kwenda kufanya tukio lile na kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.

Wambura amesema, katika uchunguzi huo polisi imebaini kwamba Hamza alikuwa akiishi kisiri huku akiwa amegubikwa na viashiria vyote vya ugaidi.

"Amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao ambayo inaonyesha matendo ya Al-Shabab na makundi kama ISIS yanayoendelea na wagaidi wengi hujifunza kupitia mitandao hiyo," amesema Wambura.

Amesema kwamba, kitendo alichokifanya Hamza kilikuwa ni cha ugaidi wa kujitoa mhanga.

"Tabia na matendo ya Hamza aliyapata kupitia mawasiliano aliyokuwa nayo na watu wanaoishi katika nchi zenye matendo ya kihalifu ikiwemo ugaidi hasa wa kupitia mtandao yanayojulikana kama "Radicalisation through social media)," amesema Wambura.

Kuhusu taarifa zinazodai kwamba Hamza aliwashambulia askari hao kwa sababu walimdhulumu madini yake, Wambura amekanusha na kusema katika uchunguzi huo wamebaini kwamba Hamza hakuwa na madini wala fedha katika mazingira yale.

"Hamza hakuwa na madini wala pesa na hakuwa katika nafasi yoyote ya kumiliki madini wala pesa mbali ya kwamba watu wengi wameongea kwamba alikuwa anamiliki migodi ya madini kule Chunya na maeneo ya Makongolosi uchunguzi wetu umebaini hali hiyo ya maisha ilikwisha simama muda mrefu," ameongeza Wambura.

Wambura ameongeza kuwa  taarifa ya uchunguzi huo pia imebaini kwamba Hamza alikuwa kwenye kundi la magaidi wanaoamua kuifia dini. (Mwananchi)

Post a Comment

0 Comments