Dkt.Sengati asikia kilio cha wanakijiji, asimamisha viongozi kazi

Na Anthony Ishengoma,Shinyanga

WANANCHI wa Kijiji cha Mwiseme Kata ya Solwa Wilaya ya Shinyanga kwa nyakati tofauti wameutuhumu uongozi wa kijiji akiwemo Afisa Mtendaji wa kijiji kwa ubadhirifu wa fedha za wananchi kijijini hapo ambazo wamekuwa wakizichanga kwa ajili ya ujenzi wa shule pamoja na zahanati na miradi mingine ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mwiseme Kata ya Solwa Wilaya ya Shinyanga alipofika Kijijini hapo kwa lengo la kuwasikiliza lakini pia kutoa suluhisho la changamoto walizonazo katika kijiji hicho.

Tuhuma hizo za wananchi kwa Mwenyekiti wao wa kijiji, Deus Manumba zimetolewa na wanakijiji hao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati aliyefika kijijini hapo kujionea maendeleo yao, lakini pia kusikiliza kero zao baada ya kubaini kuwepo kwa tuhuma hizo.

Jigela Salanya mkazi wa Kijiji cha Mwiseme amelalamika mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji alichangisha fedha kiasi cha sh.12,000 kutoka kwa wananchi kijijini hapo kwa ahadi kuwa atasaidia kuwapatia vitambulisho vya Taifa zikiwa ni pamoja na kugharamia usafiri kufuatilia vitambulisho vyao, lakini mpaka sasa zoezi hilo halijafanyikiwa hivyo kumtaka Mkuu wa Mkoa kumuondoa kiongozi huyo. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mwiseme Kata ya Solwa Wilaya ya Shinyanga alipofika kijijini hapo akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Philemon Sengati kwa lengo la kuwasikiliza lakini pia kutoa suluhisho la changamoto walizonazo katika kijiji hicho.

Katika hatua nyingine,Zambi Ruchambagula Jegu aliwekwa ndani na viongozi wa kijiji hicho kwa sababu ya kuhoji kuhusu kusomewa mapato na matumizi ya kijiji hicho na badala yake Mwenyekiti na watu wake walimfuata mke wake na kuiba kiasi cha shilingi laki nne na alitumia fursa hiyo kuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia ili aweze kurejeshewa fedha yake.

Kama hiyo haitoshi, Lunde Manyabili amesema Mwenyekiti huyo wa kijiji, Bw. Deus Manumba pia alishachangisha wananchi kijijini hapo fedha kiasi cha sh.13,000 ili aweze kujenga choo cha shule, lakini wakazi hao wanashangaa kuona choo hicho kimejengwa kwa miti na hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi shuleni hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati pamoja na viongozi wengine wa Mkoa wakisikiliza kero za wananchi wa Kijiji cha Mwisemo Kata ya Solwa Wilaya ya Shinyanga alipofika Kijijini hapo kwa lengo la kuwasikiliza lakini pia kutoa suluhisho la changamoto walizonazo katika Kijiji hicho.

Malalamiko hayo ya wanakijiji hayo yakamsukuma Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati kuwasimamisha kazi Mtendaji wa Kata na Mwenyekiti wa Kijiji ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.

‘’Hizi tuhuma ni kubwa mno na mimi kama msimamizi wa amani mkoa wa Shinyanga siwezi kuendelea kuvumila haya kwa hiyo ninatamka rasmi kwamba tunamsimamisha kazi Mwenyekiti, Mtendaji wapishe uchunguzi ambao utabainisha ukweli kati yenu ninyi wananchi na wao,’’ameongeza Dkt.Philemon Sengati ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Dkt.Sengati ameongeza kuwa, uchunguzi huo utaangalia suala zima la ubadhirifu wa fedha, lakini pia wa kimaadili ili ikibainika wana mapungufu kimaadili basi wachukuliwe hatua za kinidhamu, lakini kama watabainika wanakabiliwa na upotevu wa fedha basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko aliwataka watendaji katika ngazi ya tarafa, kata na vijiji kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo na kuhakikishia mapato na matumizi yanawekwa wazi kwa ajili ya wananchi kupata uelewa wa matumizi ya fedha yao.

Post a Comment

0 Comments