GST yatoa taarifa ya utafiti wa madini wilayani Nanyumbu

Na Tito Mselem, Mtwara

Wataalamu kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wametoa taarifa za utafiti wa madini walioufanya Oktoba 2020 katika kata za Chipuputa, Nanyumbu, Napacho na Masuguru wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Mkuu wa Wilaya wa Nanyumbu, Maariam Chaurembo akikabidhiwa taarifa ya utafiti wa Madini na Mjiolojia Abbas Mruma uliofanyika wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Akitoa taarifa ya utafiti huo, Mjiolojia kutoka GST, Abbas Mruma amesema utafiti uliofanyika Oktoba 2020 katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Nanyumbu umebaini hali ya uwepo wa madini ya dhahabu na madini ya ujenzi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mruma amesema chimbuko la tafiti hiyo ni kutokana na Waziri wa Madini, Doto Biteko, kuombwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali kufanyiwa utafiti wilayani humo ili wachimbaji wa madini ya dhahabu wachimbe kwa uhakika na waachane na uchimbaji wa kubahatisha.

Aidha, Mruma ametoa elimu kwa wachimbaji wadogo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nanyumbu juu ya matumizi sahihi ya taarifa za jiosayansi kutoka GST.
Mkuu wa Wilaya wa Nanyumbu Maariam Chaurembo (katikati) akifuatilia taarifa ya utafiti wa madini kutoka kwa Mjiolojia Abbas Mruma uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Mjiolojia Abbas Mruma kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuwasilisha taarifa ya utafiti wa madini uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Mkuu wa Wilaya wa Nanyumbu Maariam Chaurembo akifuatilia taarifa ya utafiti wa madini kutoka kwa Mjiolojia Abbas Mruma uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.

Pamoja na mambo mengine, Mruma amesema takriban sampuli 33 za miamba na udongo zilichukuliwa na kupimwa ambapo zilionesha viashiria vya uwepo wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Lukwika.

“Niwaombe wamilki wote wa leseni mtumie taarifa zinazotolewa na wataalamu kutoka GST zinazo onesha uwepo wa mashapo na uelekeo wa miamba katika maeneo yenu ili mchimbe kwa faida,” amesema Mruma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mariam Chaurembo amewataka wachimbaji wote wilayani humo kuchimba kwa kufuata Sheria na Taratibu ikiwemo kukata leseni za uchimbaji na biashara za madini.
Mjiolojia Abbas Mruma kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) akizunguza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha taarifa ya utafiti wa madini uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Baadhi ya washiriki walioshiriki kikao cha kuwasilisha taarifa ya utafiti wa madini uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Mchimbaji Mdogo wa Madini ya dhahabu Ramadhani Mtafuni akisaini kitabu cha wageni katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya utafiti wa madini uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara Mushi akizungumza jambo katika kikao cha kuwasilisha taarifa ya utafiti wa madini uliofanyika Wilayani Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.
Pia, Chaurembo amewashauri wachimbaji wa madini wilayani humo kuachana na mambo ya kupiga ramli ili wapate madini na badala yake wazitumie taarifa za GST ili waachane na kuchimba kwa kubahatisha.

Vilevile, Chaurembo ameagiza wafanyabiashara wote wilayani humo kulitumia soko la madini la Wilaya ya Nanyumbu baada ya kugundua kwamba, kuna baadhi ya wachimbaji wanauziana madini ya dhahabu nje ya soko.

“Nichukuwe fursa hii kuiomba Wizara ya Madini kuleta wataalamu wa madini katika wilaya yetu ili watusaidie katika kutupa elimu ya madini katika maeneo ya uchimbaji pia, niombe GST kupunguza gharama za utafiti ili wachimbaji wangu waweze kumudu gharama za tafiti,” amesema Chaurembo.

Kufuatia hatua hiyo, Chaurembo amesema madini ni rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia Tanzania ambapo amesema ipo siku madini hayo yataisha hivyo amewataka wachimbaji wachimbe kwa utaratibu ili yainufaishe Nanyumbu na nchi kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news