HAMASISHENI MARIDHIANO KUJENGA AMANI-OTHMAN

NA MWANDISHI MAALUM

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kuhamasisha maridhiano ya kisiasa na ya kijamii, ili kujenga amani ya kweli katika nchi.
Mheshimiwa Othman ameeleza hayo leo ofisini kwake Migombani Mjini Unguja, alipokutana na Ujumbe wa Shirikisho la Jumuiya za Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) uliofika kujitambulisha na kujadili changamoto zinazowakabili.

Amesema kuwa, maridhiano ni mtaji na raslimali muhimu inayopelekea kupatikana kwa amani, na endapo yakitoweka nchi haiwezi kuimarika, na hatimaye huleta machafuko yanayoweza kuongeza kasi ya mahitaji maalum na hata ongezeko la watu wenye ulemavu.

“Hapa ninapenda niwape changamoto kidogo kama ilivyo kwa jumuiya nyingine, mkahamasishe maridhiano yatakayopelekea ujenzi wa amani ya kweli kama ajenda muhimu, kwani yakija machafuko siyo tu yatawaathiri watu wenye ulemavu, bali yataongeza hata huo ulemavu wenyewe,"amesisitiza Mhe. Othman.

Mheshimiwa Othman amebainisha zaidi mambo yanayochangia wimbi la ulemavu, ambayo ni pamoja na ongezeko la maradhi yasiyoambukiza, dawa za kulevya, na makosa ya uzembe wa usalama barabarani.

Kwa upande wao viongozi wa SHIJUWAZA, Makamu Mwenyekiti na Mratib, Bw. Ali Omar Makame na Bakar Omar Othman, wameeleza kuwa, uwepo wa Shirikisho hilo ni juhudi za makusudi za kupigania haki, fursa na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu, ili kuimarisha ustawi bora wa jamii katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Viongozi hao wamezishukuru Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ya Zanzibar, kutokana na kuungamkono juhudi za kuwakomboa watu wenye ulemavu nchini, licha ya changamoto nyingi zinazowakabili zikiwemo za udhalilishaji na ugumu wa maisha.

Kikao hicho kiliwajumuisha viongozi mbali mbali pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dkt Omar Dadi Shajak, ambaye amebainisha juhudi zinazochukuliwa na Wizara husika za pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kutekeleza azma ya ushiriki unaostahiki wa mikutano ya kitaifa na kimataifa, inayowajumuisha watu wenye ulemavu.

Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe Othman Masoud Othman, amekutana na Uongozi wa Taasisi ya Kuwasaidia Vijana kupata Fursa za Masomo Nje ya Nchi (STUDY- ABROAD) na kushukuru juhudi muhimu wanazozichukua katika uwezeshaji wa kitaalamu kwa vijana, na kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.

Mhe Othman amesema kuwa ubunifu uliotekelezwa na taasisi hiyo ni hatua muhimu ya kupongezwa, hasa kutokana na uwezo mdogo wa serikali, wa kumhudumia kila kijana anayehitaji udhamini wa masomo, ndani na nje ya nchi.

“Nataka nieleze shukrani zangu za dhati kwa ‘initiative’ hizi mlizoanzisha, tukizingatia kuwa hali ya maisha inabadilika hasa kutokana na ushindani wa soko la ajira katika ngazi za kitaifa na ulimwenguni kote, naamini ‘the more we get quality education, the more we set to win the global competitive employment market”, alisema Mhe Othman.

Naye, Meneja wa ‘STUDY ABROAD’ Bw Yussuf Mohamed Suleiman, ameiomba Serikali kuzidisha mashirikiano na taasisi yake, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazowakabili ambazo ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii katika upatikanaji wa fursa za masomo nje ya Nchi, upotoshaji wa taarifa, na gharama kubwa za tozo katika huduma za usahihishaji wa vyeti na pia za vipimo vya Maradhi ya Corona (COVID-19).

Meneja huyo aliambatana na viongozi mbali mbali pamoja na Mlezi wa Taasisi hiyo, Dkt Sira Ubwa Mwamboya, ambaye alipongeza fursa muhimu pamoja na zile zinazotolewa na Serikali, za kuwawezesha vijana kujiendeleza kielimu, kwaajili ya maendeleo ya Nchi na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments