HOPE FOR GIRLS AND WOMEN IN TANZANIA WAFANYA BONANZA LA MICHEZO KUELIMISHA JAMII MADHARA YA UKATILI WA KIJINSIA WILAYANI SERENGETI

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania ( HGWT) la mkoani Mara linalojihusisha na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia limefanya bonanza maalumu la michezo mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha wanananchi Wilaya ya Serengeti wawe mabalozi wa kupinga mila na desturi zenye madhara kwa watoto wa kike ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni ambazo huwafanya wasitimize ndoto zao.
Bonanza hilo limefanyika Septemba 4 , 2021 katika viwanja vya Polisi Mugumu na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, mashirika binafsi pamoja na mabinti wa Nyumba Salama Serengeti na Mugumu wanaohifadhiwa na shirika hilo chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly.

Mkurugenzi wa shirika, hilo Rhobi Samwelly amesema lengo la kuandaa bonanza hilo ni kuifikishia jamii ujumbe wa kutambua madhara ya ukatili wa kijinsia na namna na kuunga mkono jitihada za serikali na mashirika mbalimbali yanayopinga vitendo vya kikatili ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na haki za binadamu.
Mkurugenzi wa ( HGWT) Rhobi Samwelly akiwa na wachezaji wa timu ya Nyumba Salama Mugumu na Nyumba Salama Butiama baada ya kumalizika kwa mchezo wa mpira wa miguu uliokutanosha Wasichana hao wanaohudumiwa na Shirika hilo kufuatia kukimbia Ukatili wa aina mbalinbali ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao.
Bonanza hili kwa hakika limefikisha ujumbe kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali na mashirika yanayopingana na vitendo vya kikatili ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni ambavyo bado vipo katika jamii. Kila mmoja wetu awe balozi wa kupinga mila hizi kwani hukwamisha ndoto za watoto wa kike kusoma na kufikia malengo yao. Pia ukeketaji una madhara mengi ikiwemo hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza, madhara ya kisaikolojia na hata ulemavu wa kudumu na kifo tuwasomeshe kusudi waje kuleta maendeleo katika jamii na taifa," amesema Rhobi.

Afisa Usitawi wa Jamii wa Wilaya ya Serengeti, Judith Petro amesema, bonanza hilo mbali na kutoa hamasa kwa jamii kupinga vitendo vya kikatili pia limechochea kutambua wasichana hao vipaji mbalimbali vya michezo walivyo navyo na hivyo kuna jukumu kubwa la kuviendeleza. Huku akiwaasa wananchi kuwa mabalozi wa kufichua wahusika wanaofanya vitendo hivyo sheria ichukue mkondo wake.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Serengeti Judith Petro akizungumza katika bonanza la michezo lililoandaliwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa Jamii kuhusu madhara ya Ukatili wa kijinsia.
Sijali Nyambuche ni Afisa Dawati la Jinsia na Watoto ambaye pia amehudhuria bonanza hilo amewaomba wananchi kutoa taarifa za vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa hususani Watoto na wasichana kusudi waweze kusaidiwa wafikie ndoto zao.

Hapines Joseph ni binti anayeishi Kituo Cha Nyumba Salama Kiabakari Wilaya ya Butiama ameshukuru uongozi wa shirika la HGWT kwa kuandaa bonanza ambalo limewaleta pamoja baina ya wananchi, viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali na kwamba litaleta ufanisi katika kuleta mtazamo chanya juu ya uwezo waliona Watoto wa kike iwapo wakitengenezewa Mazingira rafiki ya kusoma badala ya kukwamishwa na kuozeshwa kwa lazima chini ya umri usio kubalika kisheria.
Neema Justine ni Mkazi wa Mugumu amesema bonanza hilo liwe chachu ya kuiamsha jamii kupambana na ukatili hususani maeneo ya vijijini ambako bado kuna mila na desturi kandamizi zinazowakabili wanawake na mabinti na kukosa sauti ya Kufanya maamuzi mbalimbali yanayowahusu.

Pius Martine mkazi wa Kata ya Geitasamo wilayani Serengeti mkoani Mara, amewaomba wazee wa kimila kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuacha kuendekeza mila ya ukeketaji na badala yake wawe sauti ya kushawishi jamii kuwajibika kufanya shughuli za uzalishaji mali na kukemea mila hiyo iliyopitwa na wakati na kwamba inamadhara makubwa kwa mabinti.

Washindi upande wa mchezo wa mpira wa Miguu timu ya Wasichana wa Nyumba Salama Butiama walikabidhiwa zawadi ya Mpira, kikombe pamoja na fedha kwa wachezaji waliofanya vizuri. Huku Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly akiahidi kulifanya kila mwaka Ili kuwaleta pamoja wadau na Serikali kujadili njia bora za kukomesha vitendo hivyo.

Post a Comment

0 Comments