Kijana achoma nyumba ya Mjane moto kisa wivu wa mapenzi

Na Hadija Bagasha, Tanga

DIRAMAKINI Blog inasisitiza kuwa, jambo la namna hii halikubaliki katika jamii, vijana mnapaswa kujiheshimu ili heshima yenu iweze kuwa na faraja, upendo na umoja kwa jamii na si kuharibu.

Rai hiyo inakuja baada ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Kidaone mkazi wa Jiji la Tanga kuchoma moto nyumba ya mjane, Frida Kasumbwe na kumtia hasara kwa kile kinachodaiwa ni kutokana na wivu wa mapenzi ya binti ambaye alikuwa akikaa nyumba moja na mjane huyo.
Muonekano wa nyumba iliyoteketea ya Mjane huyo
Mjane Frida Kasumbwe akibubujikwa na machozi baada ya tukio hilo.

DIRAMAKINI Blog ambayo imeshuhudia tukio hilo la kuchomwa nyumba moto, limetoka eneo la Mikanjuni jijini Tanga majira ya saa nane za usiku baada ya Kidaone kumwagia mafuta ya petroli nyumba hiyo kwa madai ya wivu wa mapenzi.

Kwa nyakati tofauti,wapangaji wa nyumba hiyo wamesema wamesikitishwa na kitendo hicho cha kinyama kilichofanywa na kijana huyo na kuiomba Serikali iwasaidie kupata haki zao za mali zao ambazo zimeteketea zote na moto, lakini pia isimamie sheria ipasavyo ili kumnusuru mjane huyo.

Saumu Hassan ambaye ni mpangaji katika nyumba hiyo amesema, baada ya kufungua mlango alimkuta kijana huyo ameshika dumu la lita 20 lenye mafuta ya petroli ambapo baada ya muda mfupi alianza kusikia kelele za mtu akilia kuwa anakufa.

"Muda mfupi nilisikia sauti kama ya maji yanamwaga na baada tu ya hapo nikaanza kusikia harufu ya petroli, ndio nikawaambiwa watoto wangu tutoke nje kutoka tu moto ulikuwa umeshasambaa ndipo mimi nikapoteza fahamu nakuja kuzinduka niko hospitali,"amesisitiza Mpangaji huyo.
Mahamudu Ramadhani ambaye ni mpangaji mwingine emesema, wamelipa kodi zao juzi tu katika nyumba hiyo na hawana uwezo wa kwenda sehemu nyingine hivyo serikali iwasaidie suala hilo ili wapate haki zao za kulipwa vitu vyao.

Mjane huyo Frida Kasumbwe katika mazungumzo na DIRAMAKINI Blog ameiomba Serikali iingilie kati ili aweze kupata haki yake.

"Mimi hapa nilipo ni mjane na sina uwezo tegemezi langu kubwa ilikuwa ni hapa ikipatikana senti zinatisaidia katika kula na mambo mengine, lakini kutokana na hali hii na kuwa kama nimechanganyikiwa naiomba Serikali inisaidie kwa kuwa sielewi vitu vya watu vimeteketea, mume wangu amefariki juzi tu hata 40 pia bado,"amesema Mjane huyo.Naye Stella Kasumbwe ambaye ndiye binti aliyesababisha nyumba hiyo kuchomwa moto na kijana aliyekuwa mpenzi wake amesema kuwa, wazazi wa kijana huyo wamemtengezea cheti kijana wao kinachoonyesha kuwa ana matatizo ya akili kitendo ambacho Stella amedai si cha kweli na kuiomba serikali kumchukulia hatua kali.
"Huyu kijana kweli nilikuwa na mahusiano naye, lakini nilipoona tabia zake sio niliamua kuachana naye na hilo neno la kuchoma nyumba moto halijaanza leo wala jana amekuwa akinifuata mpaka kazini kunifanyia matukio ya fujo huku akiahidi kunifanyia tukio ambalo sitokaa nilisahau katika maisha yangu,"amesema.

Hoja yake ikaungwa mkono na Veronica Pius ambaye ni mama mdogo wa Stella anasema, "Huyu kijana amekuwa akifanya matukio mbalimbali akitegemea kuwa baba yake ana uwezo mkubwa akikamatwa wakati wowote anatoka, hivyo tunaomba suala hili litazamwe,"amesema.Aidha, jitihada zaidi zinaendelea ili kuujua ukweli kutoka kwa wazazi wa mwanaume na hata kwa upande wa Jeshi la Polisi, hivyo endelea kufuatilia DIRAMAKINI BLOG kwa UhakikaZaidiSaa24.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news