Mheshimiwa Bashungwa: Fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati barabara jimboni zitumike kulingana na malengo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali imetoa shilingi milioni 700 kusaidia ukarabati wa barabara za vijijini katika Jimbo la Karagwe mkoani Kagera ili kuboresha miundombinu ya jimbo hilo, hatua inayosaidia kurahisisha mawasiliano na kuboresha huduma za kijamii jimboni humo.
Akiwa ziarani jimboni humo kukagua miundombinu ya barabara zinazokarabatiwa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati wa barabara jimboni humo zitumike kulingana na malengo yaliyokusudiwa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa.

Bashungwa amewahimiza wabunge wenzake mkoani Kagera kuwa mstari wa mbele kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha barabara za vijijini zifanye kazi iliyokusudiwa kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi kwa kuboresha uchumi wao na taifa kwa ujumla.

“Sisi tunamshukuru Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutupa kiasi hiki kikubwa cha fedha ili tuboreshe barabara kwenye majimbo yetu lakini wito wangu ni kwamba hawa wataalumu wasisubiri mbunge aende site ili kuwaambia eneo fulani mlitakiwa muweke mataleo au mitaro ya maji ili yasiaharibu barabara, wataalamu wenyewe wanatakiwa wajue tangu wanaposanifu ujenzi husika,"amesema Mhe. Bashungwa.

Akizungumzia hatua hiyo Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Karagwe, Bw. Kalimbula Malimi amesema baada ya ziara hiyo sehemu zote zilizoainishwa ambazozinahitaji marekebisho zitafanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Katika ziara hiyo Bashungwa aliambatana na Madiwani wa kata mbalimbali, watendaji wa TARURA na TANROADS ambapo ameeleza kushtushwa kwake na namna mkandarasi anayetekeleza ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilometa 96 inaanzia kata ya Nyakahanga kwenda kata za Nyabiyonza, Bweranyange, Nyakakika, Nyakabanga, Kibondo mpaka Lukanja ambayo imejengwa bila kuweka matoleo ya maji na mitaro ya barabara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa wilaya ya Karagwe akiwemo diwani wa Kata ya Nyakakika, Exsavery Buguzi wameeleza matarajio yao kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza urahisi wa shughuli za biashara kwa maana ya usafiri na kusafirisha mizigo kati ya wakazi wa mkoa wa Kagera na nchi jirani ya Rwanda kupitia kivuko cha Bweranyange ambacho kinaziunganisha nchi hizo mbili kwa usafiri wa majini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news