Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki wawakutanisha wakuu wa mikoa jijini Tanga

Na Hadija Bagasha, Diramakini Blog

NAIBU Waziri Nishati, Stephen Byabato amesema kwamba mpaka sasa Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya EACOP wamelipa fidia ya Shilingi Bilioni 2.886 ya ardhi kwenye maeneo ya vipaumbele vya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga.
Byabato ameyasema hayo leo mjini Tanga wakati akifungua Semina ya Wakuu wa Mikoa kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.
Naibu Waziri Byabato amesema kwamba wananchi 351 tayari wamelipwa katika maeneo 14 ya vipaumbele vya mradi wanayoyaita hivyo, kwa sababu ni kwenye zile kambi ambapo shughuli mbalimbali zitakuwa zinafanyika.

Amesema, ile mkuza au njia ya kupitisha bomba fidia yake itakuja baade kidogo, lakini zile Bilioni 2 na milioni 286 ni kwa ajili ya maeneo walioyachagua itafanyika shughuli hiyo kwa mfano Tanga, Tabora,Manyara na maeneo mengine kama hayo.
Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato akizungumza wakati wa Semina ya Wakuu wa Mikoa kuhusu fursa zitakazopatikana kutokana na mradi wa ujenzi wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.(Picha na Hadija Bagasha Tanga).
Naibu Waziri huyo amesema, malipo ya fidia kwenye maeneo ya mkuza yanatarajiwa kulipwa mwishoni mwa mwaka huu 2021 huku akieleza kwamba ujio wa mradi wa Bomba la Mafuta utafungua fursa ya ajira zaidi ya 10,000 kwa kipindi cha miaka mitatu ya ujenzi.

Hata hivyo, amesema Rais Samia Suluhu amekuwa akiwaasa kila wakati kuwa wahakikishe wanawapa elimu wananchi juu ya mradi huo wa bomba la mafuta na namna watakavyoweza kunufaika.

“Hivyo ni matumaini yangu kwamba wadau na wengine kutoka taasisi binafasi na wananchi wenu mtajipanga kuhakikisha mnazitumia vema fursa kwa lengo la kunufaika kupitia mradi huo,"amesema.

Awali akizungumza wakati wa semina hiyo,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dastan Kitandula aliishukuru Serikali na kuahidi kuwa bunge litaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha mradi huo unakamilika na kunufaisha Taifa.
Dastan Kitandula ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. "Bunge lipo pamoja na Serikali na tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanikisha mradi huu mkubwa ambao utanufaisha Taifa letu na kuleta ajira nyingi kwa wananchi wetu,”amesema Kitandula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Naghenjwa Kaboyoka amesema kuwa, lengo ni kuhakikisha bomba hilo la mafuta linafikia Tanzania kama Serikali ilivyokusudia.

“Viongozi ambao bomba hili litapita kwao wasimamie vizuri bomba la mafuta katika sehemu linapopita, kwani sisi tunasema fedha za walipa kodi na sisi tutakuwa tunasimamia fedha ambazo serikali imepewa wajibu kuzisimamia matumizi yake na sisi tutakuwa jicho kwa wapiga kura wetu watanzania kwa kujua fedha zimetumikaje,”amesisitiza Kaboyoka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya, Hesabu za Serikali, Naghenjwa Kaboyoka.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga, Henry Shekifu akizungumza katika semina hiyo.

Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Mwenyekiti chama cha CCM mkoani Tanga  Henry Shekifu amesema kuwa Rais Samia amewapa heshima kubwa ya kumteua Waziri wa Nishati kutoka mkoani Tanga.

Shekifu amesema kuwa, anawatakia heri ya kufanya vizuri kwa kile wanachokitekeleza kwani ilani yao imejikita katika kutimiza mahitaji ya wananchi, hivyo kutokana na chama hicho kukomaa kisiasa hakina wasiwasi ila watendaji ndio wanapaswa kusimamia na kufanyia kazi utekelezaji maendeleo ya wananchi yanayotekelezwa na serikali.

“Tanga ni moja kati ya mikoa tajiri ilikuwa ni mkoa wa pili katika kuipatia serikali mapato ambapo yalishuka baada ya zao la mkonge kupungua uzalishaji ila kupitia bomba hili la mafuta litaifanya Tanga mbali na kufunguka kiuchumi, lakini pia litaifanya Tanga kuwa ya kihistoria,”amrsema Shekifu.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa Tanga, Adam Malima amesema, Tanzania ina miradi mikubwa miwili ikiwemo mradi wa SGR, na Mradi wa Stigglers George ambapo mradi wa tatu ni mradi huo wa bomba la mafuta, hivyo ni vyema wakawa na uelewa wa pamoja wa sasa na wa baadae, lakini pia ipo haja ya wakuu wa mikoa kupata taarifa za maendeleo katika kila hatua inayotekelezwa.

“Tanga tuna miradi mitatu mikubwa ambapo mradi wa kwanza ni wa upanuzi wa bandari ya Tanga, ambao unakwenda kuingia ushindani na bandari ya Mombasa, mradi wa pili ni Airport Tanga, na Reli ambayo ni miradi ya kimkakati na itafungua uwezo wa kupeleka mizigo maeneo mbalimbali ambapo mikoa zaidi ya 8 itanufaika na miradi hiyo,”amesema Malima.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio amesema shirika hilo litahakikisha kwamba hatua zote za mradi zinakamilika na unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili uweze kuleta tija kwa Taifa.

Bomba hilo litapita kwenye mikoa nane ya Tanzania Bara,wilaya 24,Vijiji 257 na Kata 134 na litasafiri umbali wa kilomita 1443 kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani huku kilomita 1147 zipo Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news