Mwalimu Makuru awapa UVCCM mbinu za kuupa kisogo umaskini

Na Fresha Kinasa Diramakini Blog

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Mwalimu Makuru Lameck Joseph ametoa wito kwa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Musoma Mjini kubuni miradi ambayo itaiingizia kipato jumuiya hiyo na kuwaletea maendeleo Vijana. Makuru ameyasema hayo leo Septemba 12, 2021 wakati akitoa mada katika Kongamano la Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) lililofanyika katika ukumbi wa chama hicho Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara.

Amesema kuwa, jumuiya hiyo ikiwa na miradi itakuwa chachu ya maendeleo na kuwezesha shughuli mbalimbali za maendeleo ya jumuiya kufanyika pamoja na maendelo ya kijana mmoja mmoja katika maisha yao. Huku akihimiza chama kiwe na vituo vya vijana vya kiuchumi vitakavyowasaidia kupata elimu ya kiuchumi na mitaji kwenye kila wilaya.
"Vijana ni injini ya maendeleo ya jumuiya na chama katika uchumi wa nchi yetu, vijana lazima mjitambue na kufanya kazi kwa bidii na kuwa na malengo chanya. Ni muhimu kuachana na uzembe badala yake kuwajibika kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa jumuiya yetu na Taifa pia,"amesema Mwalimu Makuru.
Amewataka vijana kujiamini na wawe mstari wa mbele kukemea maovu ikiwemo udokozi wa mali za umma na usimamizi mbovu wa miradi ya Serikali. Huku akiwaasa viongozi vijana walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuzitumia vyema nafasi hizo katika kuwaletea maendeleo wananchi maeneo walipo.

Kwa upande wake Daktari Muniko amewaasa vijana kuepuka utumiaji wa madawa ya kulevya pamoja na unywaji wa pombe sambamba na kujiepusha kufanya ngono zembe ambazo hupelekea kupata magonjwa ya kuambukiza na kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Aidha, amewahimiza kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuendesha vyombo vya moto kwa kasi isiyotakiwa pamoja na kujenga tabia ya kutumia huduma za afya mara kwa mara kikamilifu kwa manufaa yao na kuzingatia mahusiano mema.
Kwa upande wake MKUU wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule amewataka vijana kutokuwa waoga kujitokeza kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na Serikali ambapo amesema Serikali ina fedha nyingi za kuwapa vijana kwa njia ya mikopo katika vikundi kupitia halmashauri, lakini baadhi ya vijana wamekuwa waoga wa kuthubutu kujitokeza kukopa ili wafanye kazi za uzalishaji kwa maendeleo yao na taifa pia.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Musoma Mjini, Hassan Milanga amewataka vijana kuzingatia maadili na kanuni za chama hicho na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo havikubaliki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Benedictor Magiri ameshukuru waandaaji wa kongamano hilo kwani limewaleta pamoja vijana na akawahimiza kushikamana, kupendana na kujituma kwa bidii kufanya kazi za maendeleo yao na kukitumikia chama pia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news