Mwenyekiti CCM Mara awataka vijana wasitumike na wenye nia ovu, awataka kumuunga mkono Rais Samia

Na Fresha Kinasa,Diramakini Blog

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (No.3) ameutaka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani humo kuyasema kwa wananchi mambo yote mazuri yanayotekelezwa na Serikali ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (No.3) katikati akizungumza na vijana wa UVCCM Wilaya ya Musoma Mjini (hawapo pichani), kushoto kwake ni Abubakar Ghati Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara.
Sambamba na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazofanya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia Sekta ya Utalii.

Ameyasema hayo leo Septemba 12, 2021 wakati akizungumza na UVCCM Wilaya ya Musoma Mjini katika ofisi za CCM Mkoa wa Mara zilizopo Manispaa ya Musoma, ambapo kongamano la vijana limefanyika, huku akisisitiza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ambazo amekuwa akizifanya kwa manufaa ya Watanzania zinapaswa kuungwa mkono na kila mwananchi.
Kiboye amesema kuwa, vijana ndani ya chama hicho wana nafasi kubwa sana ya kuhakikisha wanakisemea chama kwa wananchi na kushiriki kujibu hoja za baadhi ya watu wanaobeza kazi zinazofanywa na Serikali bila kuwaogopa katika maeneo yao. Huku akiwataka kutokubali kutumiwa vibaya na baadhi ya watu kwa masilahi yao binafsi.
"Vijana simameni imara kukipigania chama, mchango wenu ni muhimu sana kwa uhai wa chama chetu, msikubali hata kidogo kutumiwa na watu wenye nia ovu. Kisemeeni chama vizuri kwa wananchi na tumuunge mkono kwa pamoja Rais Samia Suluhu Hassan kwa yale yote anayoyafanya kwa ajili ya Watanzania ikiwemo kuitangaza nchi Kimataifa kupitia utalii ambao ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo,"amesema Kiboye.

Katika hatua nyingine, Kiboye amesema chama hicho ni thabiti na imara n kina umoja na mshikamano tofauti na miaka ya nyuma ambapo makundi yalikuwepo kwa kiasi kikubwa na hivyo amewahakikishia wana CCM wote kuwa chaguzi ndani ya chama hicho zijazo zitafanyika kwa amani na watakaotafuta nafasi za uongozi kwa njia ya rushwa ndani ya chama hicho hawatafanikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news