Naibu Meya Manispaa ya Musoma, Haji Mtete ateta na wafanyabiashara Soko la Nyasho

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

NAIBU Meya wa Manispaa ya Musoma ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyasho, Haji Mtete amewahakikishia wafanyabiashara wa Soko la Nyasho lililopo katika kata hiyo kuwa,mpango wa Serikali wa kujenga soko hilo haujaahirishwa.
Mhe. Mtete ameyasema hayo Septemba 13, 2021 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko hilo ambapo baadhi yao walitaka kujua iwapo ujenzi wa soko hilo utafanyika kama walivyoahidiwa kipindi cha nyuma, ukiwa ni mwendelezo wake wa kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.

Amesema, soko hilo ni miongoni mwa miradi ambayo imeombewa fedha na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa wafadhili ukiwemo mradi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 14 na mwalo wa Makoko na kwamba, hatua mbalimbali zimekwishafanyika za kufanya uhakiki wa miradi hiyo na baada ya fedha kutolewa ujenzi wa soko hilo utafanyika.

"Tulipata fedha za ufadhili kutoka Benki ya Dunia ambapo zilijenga barabara za lami katika Manispaa yetu na kupendezesha kwa hali nzuri sana na Kata ya Nyasho ilinufaika na mradi huo kwa kiwango kikubwa sana. Katika awamu hii ipo miradi ambayo pia itatekelezwa baada ya fedha kutolewa kama ambavyo iliainishwa tuendelee kumuomba Mungu fedha zitolewe mapema soko letu lijengwe, hivyo dhamira ya Serikali iko palepale tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu afanikishe,"amesema.

Pia, amewataka kuendelea kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ikiwemo kuwa waaminifu kulipa kodi za Serikali ili kuiwezesha kutoa huduma mbalimbali za kijamiii kwa wananchi. Akawaomba wazidi kumuamini kwani hatawaangusha katika kuwatumikia Kama ambavyo ilani ya CCM inamtaka kuwajibika kwa wananchi.

Neema Paul ni mfanyabiashara wa soko la Nyasho ambapo amesema, iwapo serikali itakamilisha ujenzi wa soko hilo Mazingira ya biashara yatakuwa mazuri tofauto na ilivyo sasa ambapo baadhi ya vibanda vimechakaa na wakati wa mvua huvuja.

"Soko likikamilika watu wengi watafanya biashara na kujikwamua kiuchumi na pia Serikali itapata mapato ya kutosha kwa ajili ya maendeleo,"amesema Neema Paul.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news