NHIF yawapa heshima maalum waandishi wa habari Tanzania Bara na Visiwani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesisitiza kuwa, utaendelea kushirikiana bega kwa bega na waandishi wa habari vikiwemo vyombo vyote vya habari nchini kwa kuwa,hao ni wadau muhimu katika kuwaunganisha na WATANZANIA ambao wamekusudia kuwapa uhakika wa matibabu bora.
Hayo yalibainishwa Septemba 24, 2021 na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa NHIF, Anjela Mziray wakati akiwakaribisha wawakilishi mbalimbali kutoka vilabu vya waandishi wa habari kupokea vyeti maalum vya kutambua mchango wa waandishi wa habari nchini katika kuhamasisha kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo bima ya afya.

Mkutano huo kati ya NHIF na waandishi wa habari kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ulifanyika kwenye Ukumbi wa LAPF jijini Dodoma kwa lengo la kupeana mrejesho wa huduma za mfuko kwa kuangalia ulipotoka, ulipo na unapoelekea na kushiriki pamoja maadhimisho ya miaka 20 ya mfuko huo ulioanzishwa 2001.

"Miaka 20 ya NHIF...Uhakika wa Matibabu kwa Wote, ndugu zangu wanahabari kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, tunawashukuru sana kwa kuweza kufika katika huu mkutano muhimu ambao unatoa tathimini na kujadili miaka 20 toka NHIF ianzishwe. Mmekuwa wadau muhimu sana kwetu, na tutaendelea kushirikiana nanyi wakati wowote, NHIF inathamini sana kazi zenu,"amesema. 

Amesema, huduma za mfuko zimesambaa nchini kote, hivyo ushirikiano na waandishi wa habari kutoka kila kona ya nchi utasaidia kuwapa elimu wananchi ili waweze kuzitumia huduma za NHIF kwa faida zaidi

Pichani chini ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa mfuko huo, Charles Lengeju akimkabidhi vyeti kwa wawakilishi mbalimbali wawakilishi wa vilabu vya waaandishi wa habari kutokana na mchango wao mkubwa wa kutoa elimu kuhusiana na mfuko huo tangu uanzishwe mwaka 2001.
Wakati huo huo, Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo ametumia nafasi hiyo kuwapongeza NHIF kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari nchini, kutokana na michango yao ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na huduma wanazotoa pamoja na kuzitangaza huduma zao.

Mbali na hayo, Nsokolo aliendelea kuwahamasisha waandishi wa habari kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili nao wawe miongoni mwa wanufaika wa huduma bora za afya nchini.

Amesema kuwa, kupitia vilabu vyao ni rahisi zaidi kujiunga na NHIF, hivyo viongozi wa vilabu kote nchini waendelee kuwa mstari wa mbele kuwapa elimu wanachama wake ili kutambua umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kutoka NHIF.

Amesema kuwa, pia wataendelea kushirikiana na NHIF kuendelea kutoa elimu iwe mijini au vijijini ili jamii iweze kutambua umuhimu wa kujiunga na bima ya afya ambayo ina faida nyingi katika maisha ya kila siku.

Post a Comment

0 Comments