Rais Dkt.Mwinyi aongoza maziko ya Jaji Haji Omar Haji

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo ameongoza maziko ya Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Jaji Haji Omar Haji yaliyofanyika Shakani, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiweka mchanga katika kaburi la Marehemu Jaji ya Mahakama Kuu Zanzibar, Haji Omar Haji, maziko yaliofanyika katika Kijiji cha Shakani Wilaya ya Magharibi ‘B’Unguja leo Septemba 12, 2021.(Picha na Ikulu).

Viongozi mbalimbali wamehudhuria katika maziko hayo akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu pamoja na viongozi wengine wa vyama vya siasa, dini na serikali, wananchi na wanafamilia.

Mapema Alhaj Dkt. Mwinyi alijumuika pamoja katika hitma na sala ya kumsalia Marehemu Jaji Haji Omar Haji huko katika Masjid Noor, uliopo Kombeni, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini Magharibi sala ambayo iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kabih.

Akisoma Wasifu wa Marehemu Jaji Omar Haji, mara baada ya maziko ya Marehemu, Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed amesema kuwa, Marehemu amezaliwa Aprili 04, 1967 huko Wilaya ya Mafia katika Mkoa wa Pwani, Tanzania Bara.

Amesema kuwa, Marehemu ameanza Elimu yake ya Msingi kuanzia darasa la Kwanza hadi darasa la Saba mwaka 1978 hadi 1984 huko Mafia na mnamo mwaka 1985 alihamia Zanzibar na kujiunga katika Skuli ya Msingi Kiembesamaki kwa kuendelea na elimu yake hadi mwaka 1987.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mnamo mwaka 1988 hadi 1991 Marehemu alianza Elimu yake ya Sekondari katika Skuli ya Vikokotoni, na kuendelea na masomo yake ya Kidato cha Tano na Sita mnamo mwaka 1993 hadi 1995 katika Skuli ya Sekondari ya Lumumba.

Mwaka 1997 hadi mwaka 1999 Marehemu alijiunga na Chuo cha Mzumbe kwa masomo ya Stashahada ya Sheria na mwaka 2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria na mnamo mwaka 2008 alisoma Shahada ya Uzamili ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch nchini Afrika Kusini.

Akimuelezea katika nafasi zake za kazi alizopitia Marehemu Haji Omar Haji, Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar alieleza kwamba Marehemu aliwahi kuwa Mwalimu wa muda katika skuli ya Sekondari ya Haile Sellasie na mnamo Oktoba 1996 aliajiriwa kazi na kuanza akiwa Karani wa Mahkama Kuu Zanzibar.

Marehemu aliwahi kuwa Hakimu wa Mkoa katika Mahakama ya Mkoa Vuga mnamo mwaka 2005 hadi 2008 wakati akiwa Hakimu wa Mkoa alipata nafasi ya kufundisha katika Chuo cha Azania.

Marehemu Haji Omar Haji aliteuliwa kuwa Naibu Mrajis Mahakama Kuu Pemba mnamo mwaka 2009-2011 na mnamo Julai 04,2018 hadi Februari 01,2021 alifanya kazi katika Mahkama ya Afrika Mashariki akiwa ni Mtendaji Mkuu wa Mhakama hiyo.

Aidha, mmano Februari 01, 2021 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar na kuapishwa Februari 2021 na mnamo Agosti 16,2021 Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alimteua kuwa Jaji Mkaazi Pemba.

Marehemu Haji Omar Haji, hadi umauti unamfika alikuwa ni Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar na Jaji Mkaazi Pemba.

Marehemu Jaji Haji Omar Haji amefariki jana Septemba 11,2021 katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja baada ya kuugua kwa muda mfupi, marehemu ameacha Kizuka Mmmoja na watoto 4, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.

Post a Comment

0 Comments