Rais Samia afanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Sudan Kusi

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 15 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini Salva Kiir Mayardit, Balozi Albino Ayuel Aboug, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mjumbe maalum kutoka kutoka kwa Rais Salva Kiir wa Sudani Kusini Balozi Albino Ayuel Aboug, aliyewasilisha Ujumbe maalum kutoka kwa Rais Salva Kiir, Ikulu Jijini Dar es salaam leo Septemba 15,2021.

Balozi Aboug amesema ujumbe huo pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit ametaka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Sudan Kusini.
Amesema Sudan Kusini inaomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua chakula kutoka Tanzania.

Aidha, Balozi Aboug amesema Sudan Kusini pindi Reli ya Kisasa (SGR) itakapokamilika ingependa kusafirishia bidhaa zake kupitia reli hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkaribisha Mjumbe maalum kutoka kwa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini Balozi Albino Ayuel Aboug aliyewasilisha Ujumbe maalum kutoka kwa Rais Salva Kiir, Ikulu Jijini Dar es salaam leo Septemba 15,2021.

Pia, amesema Sudan Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule za msingi kutoka nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kwa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kuhusu ombi la kutumia Bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news