Rais Samia atoa ajira 2,300 vyombo vya usalama

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa ajira mpya za askari 2,300 kwa vyombo vyote vya usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akizungumza katika kikao na viongozi wakuu wa utawala wa vyombo hivyo, katika ukumbi wa mikutano wa wizara uliopo Mtumba jijini Dodoma, Simbachawene amesema ofisi yake imepokea barua kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu ajira mpya.

"Jeshi la Uhamiaji limepewa nafasi 350 kwa kada ya Konstebo, lakini pia nafasi 700 kwa Jeshi la Magereza kwa nafasi za ‘Warder’ na ‘Wardress’, pia nafasi 250 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kada ya Konstebo, na pia nafasi 1,000 kwa Jeshi la Polisi kwa kada ya Konstebo,”amesema Simbachawene.

Waziri Simbachawene amesema, kwa niaba ya wizara yake pamoja na vyombo anavyoviongoza amemshukuru Rais Samia kwa kutoa nafasi hizo ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa askari katika vyombo hivyo.

“Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya wizara na vyombo hivi ambavyo wizara yetu inavisimamia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia nafasi hizi, pamoja na changamoto tulizokuwa navyo, suala la upungufu wa askari lilikua jambo ambalo linatupa changamoto, na uzuri ni kwamba kibali kilichokuja kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kimeelekeza kabisa tuajiri askari wa ngazi ya chini,” amesema Simbachawene.

Ameongeza kuwa, askari hao ndio watakuwa wapiganaji, wapambanaji na anatarajia kuwa vyombo hivyo katika mchakato wake vitazingatia maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba watakaopata nafasi hizo ni wale waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kupata malezi na kuhitimu lakini pia walishiriki katika kujenga nchi kupitia JKT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news