Rais Samia awapa ujasiri wanawake nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amewaomba wanawake nchini kushikamana ili kuhakikisha wanamchagua mwanamke kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam iliyokuwa na kaulimbiu “Ajenda ya Mwanamke ni Turufu ya Ushindi”.Amesema kwasasa Rais aliyepo madarakani amewekwa kwa kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba hivyo amewaomba wanawake kuhakikisha kuwa mwaka 2025 wanamuweka madarakani Rais mwanamke.

Mhe. Rais Samia amewataka wanawake kuhakikisha fadhila walizopewa na Mungu hawaziachii kwa kuwa wanawake wamefanya kazi kubwa ya kuleta uhuru, kujenga siasa na kuwabeba wanaume katika siasa za nchi, hivyo iwapo wataziachia fadhila hizo Mungu atawalaani.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongozwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia kama inavyotamkwa wazi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 3 (1).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wanawake pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya Siasa katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Demokrasia Duniani iliyofanyika leo tarehe 15 Septemba, 2021 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Pia amesema Tanzania inaongoza kwa Uhuru wa vyombo vya Habari kwa kuwa na vyombo vingi vya habari ambavyo kati ya hivyo asilimia 75 vinamilikiwa na watu binafsi.

Vilevile, amesema Serikali ya Awamu ya Sita itajitahidi kushughulikia masuala ya haki za wanawake na usawa wa jinsia ili kukuza demokrasia nchini, ikiwemo kutekeleza yaliyomo kwenye Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo (kama kiashiria cha Ushindi wa Mwanamke Mtanzania) kutoka kwa Mwenyekiti wa Azaki ya Tanzania Women Cross-Party Platform/ULINGO Mama Anna Abdallah kabla ya kuhutubia katika siku ya maadhimisho ya Kimataifa ya Demokrasia Duniani iliyofanyika leo tarehe 15 Septemba, 2021 katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Ikulu).

Mhe. Rais Samia amesema Demokrasia inahusiana kwa karibu na masuala ya haki ya kuishi hivyo wananchi wachukue tahadhari dhidi ya UVIKO 19 kwa kupata chanjo kwa hiyari ili kupunguza madhara yatokanayo na janga hilo ikiwa ni pamoja na vifo.

Katika maadhimisho hayo, Mhe. Rais Samia amekabidhiwa Tuzo kama kiashiria cha ushindi wa mwanamke Mtanzania iliyotolewa Azaki ya Tanzania Women Cross – Party Platform/ ULINGO.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news