Royal Family yazidi kuwekeza shule za kisasa Geita, RC Senyamule aipa kongole

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema kuwa shule ya msingi ya binafsi ya Royal Family inachangia kwa kiwango kikubwa kuunyanyua Mkoa wa Geita kushika nafasi nzuri kitaifa katika mitihani ya darasa la saba ya Baraza la mitihani Tanzania.
Madarasa mapya ya shule mpya ya Sekondari ya Royal Family iliyozinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Rosemary Senyamule (picha na Robert Kalokola).

Amesema kuwa, shule hiyo imekuwa inafanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba kitaifa kuanzia mwaka 2017 ambapo imekuwa inashika nafasi ya kwa kwanza kimkoa na imedumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Mkuu wa mkoa, Senyamule amesema hayo katika mahafali ya tano ya darasa la saba katika shule ya msingi ya Royal baada ya kumaliza uzinduzi wa shule mpya ya Sekondari ya Royal Family.

Aidha,mkuu wa mkoa huyo amesema kuwa shule imekuwa kwenye nafasi nzuri kitaifa jambo linalochangia mkoa huo kushika nafasi nzuri kitaifa wakati wa kukokotoa wastani wa jumla kwa mikoa yote nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule (mwenye koti nyeupe) akikata utepe kuzindua shule mpya ya Sekondari ya Royal Family Geita Mjini, kushoto ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Mhandisi Lazaro Philipo (Picha na Robert Kalokola).

Ameongeza kuwa, shule nyingi zimekuwa zinashika nafasi ya kwanza mara moja tu na kupromoka hadi nafasi ya pili na kuendelea lakini kwa shule ya msingi Royal Family ni tofauti kwa sababu imeweza kuhimili kudumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu.

Mkuu wa mkoa Rosemary Senyamule amesema kuwa, katika matokeo ya kitaifa kidato nne ushindi wa mkoa wa Geita umekuwa wa wastani wa asilimia kati ya asilimia 80.

Amesema, malengo ya mkoa ni kusogea hadi ushindi wa wastani wa asilimia 90 na kadri shule kama Royal Family zikifaulisha vizuri zitasaidia mkoa kufikia malengo hayo hadi kufikia asilimia 100.
Baadhi ya wanafunzi wa chekechea shule ya msingi Royal Family wakicheza mchezo wa kusaka mrembo namba moja hadi tatu (Miss Royal Family) katika mahafali ya tano ya darasa la saba (Picha na Robert Kalokola).
Mkurugenzi wa shule hiyo, Mhandisi Lazaro Philipo amesema kuwa taasisi ya Royal Family imekuwa ikimiliki shule ya msingi tu,lakini sasa wameanzisha shule ya sekondari kwa ajili ya kuendeleza vipaji vinavyotengenezwa kwenye shule yao na msingi na kutoka maeneo mengine ya nchi.
Mkurugenzi wa Royal Family, Mhandisi Lazaro Philipo akizungumza katika mahafali ya tano ya shule ya msingi Royal baada ya kuzindua shule mpya ya Sekondari ya Royal Family. (Picha Robert Kalokola).

Ameongeza kuwa, shule hiyo inaanza rasmi kidato cha kwanza mwaka 2022 na kwa sasa shule hiyo imekamilika madarasa kumi na mbili ya kuanzia, maabara, ofisi za utawala na walimu, mabweni na uzio kuzunguka shule kwa ajili ya usalama wa shule na wanafunzi.

Mkuu wa shule hiyo, Francis Odongo amesema kuwa shule hiyo imekuwa inafanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba tangu mwaka 2017 kwa kushika nafasi nzuri.
Mkuu wa Shule ya Royal Family, Francis Odongo.
Ametaja nafasi hizo kuwa katika Matokeo ya darasa la Saba Mwaka 2017 shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 7 na wote walipata daraja A na shule kushika nafasi ya 38 kitaifa, ya 3 kimkoa na ya kwanza kiwilaya.

Mwaka 2018 ilikuwa na wanafunzi 19 na wote walipata daraja A , shule ikashika nafasi ya 33 kitaifa ,ya 4 kimkoa na 2 kiwilaya.

Aidha , mwaka 2019 shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 30 wote walipata daraja A na shule ikawa ya 33 kitaifa,4 kimkoa na 2 kiwilaya.

Ameongeza kuwa mwaka 2020 shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 41 na wote walipata daraja A ,kitaifa ilikuwa ya 22,kimkoa ilishika nafasi ya kwanza na kwanza kiwilaya.

Post a Comment

0 Comments