Serikali yatoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhusiana na Wataribu wa TASAF

Na Mwandishi Wetu, Moshi

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Waratibu wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanatekeleza kikamilifu jukumu la kuratibu utekelezaji wa mpango huo ili kuiwezesha Serikali kutekeleza azma yake ya kuzinusuru kaya zote maskini nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Waratibu wa TASAF Mkoa wa Kilimanjaro (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na waratibu hao, chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi chake na Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa Halmashauri za Mkoa wa Kilimanjaro chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Waratibu hao mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amewataka Wakurugenzi hao kuwapa Waratibu wa TASAF muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu badala ya kuwabadili kila mara, kitendo kinachosababisha kutokuwa na mwendelezo mzuri wa usimamizi wa miradi ya TASAF nchini.

“Mradi wa TASAF ni mradi mkubwa sana wa kimkakati ambao unagusa moja kwa moja maisha ya mamilioni ya Watanzania wa kipato cha chini, hivyo kukiwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya waratibu yataathiri mwendelezo mzuri wa usimamizi wa miradi ya TASAF,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiongoza kikao kazi kwa Waratibu wa TASAF Mkoa wa Kilimanjaro, chenye lengo la kuwahimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa TASAF Mkoa wa Kilimanjaro mara baada ya kuhitimisha kikao kazi chake na waratibu hao, chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Ameongeza kuwa, TASAF inapeleka fedha nyingi za ruzuku kwa walengwa kwenye miradi ya maendeleo, miradi ya ajira za muda, miradi ya kuboresha sekta ya afya na sekta ya elimu hivyo, Serikali inahitaji kuwa na Waratibu watakaokuwa na muda wa kutosha wa kusimamia vizuri mchakato mzima wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kilimanjaro, iliyokuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ikiwa ni pamoja kusisitiza usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news