Wamkasirisha RC Sengati wilayani Kishapu "NINARUDI"

Na Anthony Ishengoma,Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt.Philemon Sengati amemwagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Kishapu, Bw. Emanuel Johnson kuwasilisha kwake taarifa ya kina ya wafanyakazi wake ambao kwa kiasi kikubwa wanasababisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Kishapu kutotekelezwa katika viwango vinavyotakiwa.

‘’Ninakupa jukumu ili Mkurugenzi kutuletea taarifa ya kina ya wale wote ambao unaamini ndio wanasababisha kusuasua kwa miradi ya ujenzi wa maabara pamoja na Zahanati awe Mkuu wa Idara au mtumishi, lakini pia na sisi tutachunguza kupitia vyanzo vyetu ili tuweze kuchukua hatua ya kina kubaini nani anahusika katika kushindwa kutekeleza miradi katika kiwango kinachotakiwa licha kuwa tumekuwa tukitoa maagizo ya mara kwa mara katika miradi hiyo,’’ amesema Dkt.Sengati ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akisaidia kuchanganya udongo alipofika wilayani Kishapu kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Dkt. Philemon Sengati amefikia hatua hiyo baada ya kutembelea mradi wa ukarabati wa vyumba vya mahabara katika Shule ya Sekondari Ukenyenge pamoja na mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwaweja vilivyopo Wilaya ya Kishapu na kujionea namna ambavyo ujenzi wa miradi hiyo ulivyo chini ya kiwango.

Kabla ya Mkuu wa Mkoa kutoa maelekezo hayo awali Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Emanuel Johnson alitoa utetezi wake kuwa yeye ni kama samaki mzuri aliyetumbukizwa katika kapu la samaki waliooza na kutumia lawama kitengo chake cha manunuzi na idara ya uhandisi kwamba hawana uadilifu wanakosa uzalendo katika utendaji kazi wao.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akisaidia fundi kuweka udongo wa kujengea vigae alipofika wilayani Kishapu kukagua maendeleo ya ya ukarabati wa maabara ya Shule ya Sekondari ya Ukenyenge mkoani Shinyanga.

Bw. Johnson amesema kuwa, Idara yake uhandisi ina mhandisi mmoja na wasaidizi wake wamekuwa hawana weledi wa kutosha na mhandisi mwenyewe utaalam wake ni katika fani ya barabara na anasaidiwa na mafundi mchundo ambao pia hawana taaluma ya kutosha kuweza kusimamia ujenzi katika kiwango kinachotakiwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo akionesha kutoridhishwa kwake na Kitengo cha Manunuzi cha Halmashauri hiyo alisema kuwa kitengo hicho kimekuwa kikiwasilisha makadirio makubwa ya gharama za ujenzi na ili kunusuru hali hiyo wakati mwingine analazimika kutumia makadirio ya hesabu za mafundi wa kawaida ili kufanya kazi ziende.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zuwena Omari amesema, mara kwa mara viongozi wamezuru miradi hiyo na kutoa mapendekezo kwa ajili ya kuboresha ujenzi huo lakini mpaka wanatembelea mradi huo hawaoni nia ya kweli ya uongozi wilayani Kishapu kuonesha wako makini katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akikagua ubora wa dirisha la maabara inayokarabatiwa katika Shule ya Sekondari ya Ukenyenge iliyopo Kishapu mkoani Shinyanga.

Aidha, Bi. Zuwena alibaini mapungufu katika taarifa ya utekelezaji wa miradi yote miwili kwani haoneshi mchanganuo halisi wa kazi zilizotekelezwa au ambazo hazijatekelezwa na kumwezesha msomaji kutambua mapungufu au mafanikio katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ukenyenge , Bw.Anderson Mandia amesema, ipo shida katika timu ya watumishi, lakini yeye hawezi kusema ni wapi, laikini mapungufu yaliyopo wameishayabaini katika kamati ya fedha, lakini pia katika baraza la madiwani.

Pamoja na utetezi kwa Mkurugenzi huyo, Dkt. Philemon Sengati anaona ipo haja ya yeye kuwajibika kutokana na Mkurugenzi huyo kutowasilisha taarifa ya uwepo wa watumishi ambao ni kikwazo katika utendaji kazi na kutaka viongozi wilayani Kishapu kubadilika ili kuhakisi kasi iliyopo ya uchumi wakati katika kuwahudumia wananchi.

Post a Comment

0 Comments