Waziri Kabudi afungua jengo la Ofisi ya Mashitaka Serengeti

Na Mwandishi Wetu,Serengeti

SHIRIKA la Grumeti Fund linalosaidia uhifadhi na maendeleo ya jamii Serengeti, limekabidhi jengo la kisasa la Ofisi ya Taifa ya Mashitaka Wilaya ya Serengeti, kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa, Palamagamba Kabudi akikata utepe wakati wa uzinduzi wa ofisi ya mashtaka ya taifa wilaya ya Serengeti.

Shirika hilo limetumia sh.milioni 284 kujenga jengo hilo ambalo lilikabidhiwa rasmi kwa waziri huyo mjini Mugumu, juzi.

Jengo hilo lenye ukubwa mita za mraba 288, lina ofisi tisa, ukumbi wa mikutano, jiko, stoo, na vyoo vitatu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa jengo hilo, Waziri Kabudi aliishukuru Grumeti Fund kwa uhisani huo, akisema ofisi hiyo itasogeza karibu na kuharakisha huduma za upelelezi na mashitaka.
“Mbali ya kusogeza huduma karibu kwa wananchi, ofisi hii ya mashitaka itasaidia kukabiliana na vitendo vya ujangili mkubwa na mdogo,” Profesa Kabudi alisema.

Aliongeza, “Nimefurahi kusikia pia kuwa wadau wengine wa Grumeti Fund kama vile TAWA na TANAPA watakuwa na ofisi zao katika jengo hili jipya.”

Aidha, Waziri Kabudi alisema ofisi hiyo itasaidia kuipunguzia Serikali gharama za kusafirisha mawakili, vielelezo na kuhudumia mashahidi.

Naye Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu alielezea ufunguzi wa jengo la ofisi ya Taifa ya Mashitaka Wilaya ya Serengeti kuwa ni tukio la kihistoria kwao.

“Leo ni siku muhimu kwetu. Hili ni tukio kubwa, Serengeti imekuwa wilaya ya kwanza kuwa na jengo lake la Ofisi ya Taifa ya Mashitaka. Nitumie fursa hii kuwashukuru Grumeti Fund kwa kutujengea jerngo hili,” Mwakitalu alisema.

Aliongeza kuwa wilaya ya Serengeti ina makosa mengi ya kijinai yanayohusiana na uvunjifu wa sheria za wanyamapori. Sehemu kubwa la wilaya ya Serengeti ni maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikorongo/ Grumeti na Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya IKONA.

DPP huyo aliahidi kuongeza mawakili wa Serikali na wafanyakazi wengine katika ofisi hiyo.

Shirika la Grumeti Fund limejenga jengo hilo ili kuongeza ufanisi katika ofisi hiyo ya mwendesha mashitaka.

“Grumeti Fund itaendelea kuwa mdau na mshiriki muhimu katika mfumo wa kiikolojia wa Serengeti na ustawi wa jamii katika wilaya za Serengeti na Bunda,” Meneja Mkuu wa Grumeti Fund, Noel Mbise alisema.

Kwa upande mwingine, Waziri Kabudi aliishukuru Kampuni ya Grumeti Reserves kwa kuwekeza katika utalii unaoitangaza Tanzania kimataifa.

Grumeti Rserves imeendelea kuwa mfano wa utalii unaong’ara wilayani Serengeti.

Pia Waziri Kabudi alilishukuru Shirika la Grumeti Fund kwa shughuli za kusaidia uhifadhi na maendeleo ya jamii.

Aliongeza kuwa mpango wa Grumeti Fund wa ufadhili wa kimasomo umewezesha mamia ya wanafunzi wa kike na kiume kutoka jamii jirani kunufaika na mpango huo.

Grumeti Fund ni shirika dada la kampuni ya Grumeti Reserves linalojihusisha na shughuli za uhifadhi na maendeleo ya jamii katika wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara.

Post a Comment

0 Comments