Waziri Mhagama:Tuwajali na kuwathamini watu wenye ulemavu

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka jamii kujali na kutambua uwezo na mchango wa Watu Wenye Ulemavu mahali popote walipo kwa kutoa haki sawa huku ikitokomeza vitendo vya unyanyapaa.
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati alipokuwa kwenye kikao cha wadau cha kupitia na kutoa maoni ya mwisho ya kukamilisha mwongozo wa kukuza ujumuishwaji na kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu, "Jamii Inayoongoza Katika Kuzingatia Haki,Usalama,Usawa,Huduma Bora na Jumuishi kwa Watu wenye Ulemavu".
Amesema kuwa, watu wenye ulemavu wanapaswa kuonyesha vipaji vyao,kwani Serikali kwa kushirikiana na wadau mballimbali ina wajibu wa kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza na kuwahakikishia ustawi na mahitaji yao ya kimsingi, ikiwemo ulinzi na usalama wao.

"Jamii iondokane na mawazo potofu kwamba watu wenye Ulemavu hawawezi chochote jambo ambalo sio sahihi na Sisi Serikali tunaweka mazingira kuhakikisha kuwa wanajumuishwa katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi ili kuinua ustawi na maisha yao kwa kuwafanya wawe na mchango zaidi katika maendeleo ya jamii zao na Taifa kwa ujumla.

"Licha ya hatua hizo zote, hali ya huduma na ustawi kwa Watu Wenye Ulemavu nchini na duniani kote, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji kuendelea kufanyiwa kazi ipasavyo na kama nchi, bado tunahitaji kuendelea kukuza ujumuishwaji na kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora kwa Watu Wenye Ulemavu, popote walipo, mijini na vijijini,"amesema Waziri.

Ametoa onyo kali kwa sekta binafsi ambazo zimekuwa zikitumia mgongo wa walemavu kwa kujinufaisha wenyewe na kupelekea kukosa haki zao za msingi na kwamba Serikali imejizatiti kuwa nao bega kwa bega kutetea haki zao na kuboresha miundo mbinu stahiki.

"Rai yangu kwenu washiriki wa kikao hiki, mtumie vizuri nafasi hii ambayo mmeipata ya kushiriki kwa kutoa maoni yatakayoisaidia Serikali kukamilisha Mwongozo huu mapema iwezekanavyo, kuweka misingi imara ya ujumuishwaji na uimarishaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu ili mwisho wa siku tuwe na jamii ya kitanzania ambayo ni jumuishi na inayozingatia haki, usawa, usalama na ustawi wa Watu wenye Ulemavu,"amesema Waziri.
Naye Naibu Waziri Ofsi ya Waziri mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu wenye Ulemavu,Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwapa kipaumbele watu wenye walemavu pale fursa za ajira zinapojitokeza ambapo kwa mwaka huu ajira za walimu 387 ni za wenye ulemavu.

"Tunaishukuru Serikali kwa jinsi inavyojali watu wenye ulemavu, kwa mwaka huu imetenga bilioni 1.2 kwa ajili yao na Serikali imekuwa mstari wa mbele kujenga vyuo kwa ajili ya watu wenye ulemavu kwa kuboresha miundombinu na wengi wamefanikiwa kuhitimu masomo yao na kufanya vizuri sehemu zao za kazi,"amesema Ummy.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chumbageni, Tanga, Ernest Kimaya amesema kuwa, kupitia kikao hicho ambacho kimewakutanisha wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kitaenda kuleta manufaa kwao.

Aidha,amesema kuwa kutokana na kitendo cha Serikali kuwajali watu wenye ulemavu hasa kwenye ajira, jamii imeanza kuondokana na mitazamo hasi na kutoa watoto wao nje kuwapeleka shule wakiwa na imani wanauwezo wa kufanikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news