Waziri Ummy azipa halmashauri miezi mitatu ujenzi wa madarasa

Na Hadija Bagasha, Tanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa, Ummy Mwalimu ametoa miezi mitatu kuanzia sasa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanajenga madarasa kabla ya mwaka 2021 kuisha ili kuepuka usumbufu kwa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa, Ummy Mwalimu alipokua akizungumza na wananchi na watendaji wa Kata ya Pongwe alipokwenda kukagua maendeleo na kupokea Taarifa ya maendeleo ya Kata. (Picha na Hadija Bagasha Tanga).

Pia amesema, hatarajii kuona walimu wanakoseshwa likizo yao kwa madai kuwa wanashughulikia ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza.

Waziri Ummy ameyasema hayo mkoani Tanga wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na watendaji wa Kata ya Pongwe alipokwenda kukagua maendeleo na kupokea taarifa ya maendeleo ya kata.

Waziri Ummy amesema, miezi mitatu hiyo aliyoitoa ni kuanzia mwezi huu wa 9, 10, na 11 hivyo amezitaka halamashauri zote nchini kujitathimini na kuondoa changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa haraka iwezekanavyo.

"Mwaka huu sisi kama TAMISEMI kusiwe na Second Selection (chaguo la pili) ya watoto wanaoanza form one (kidato cha kwanza) kwa mwaka 2022,tunataka kila halmashauri wajitathmini na kujua nina watoto wangapi wanaofanya mtihani wa darasa la saba keshokutwa na anategemea watoto wangapi watafaulu kuanza kidato cha kwanza,ninayo madarasa mangapi ya kupokea watoto wa kidato cha kwanza,uhaba ni mangapi,kwa hiyo tunataka madarasa yajengwe mwezi wa 9,10 na 11,"amesema.

Ameongeza kuwa, "tunataka watu waende nyumbani wakajumuike na familia zao kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya,sio kunyimana likizo tunataka kazi ikamilike ikifika mwezi wa kwanza watoto wanaenda shule kuanza kidato cha kwanza wale waliofaulu.

"Sasa mimi Ummy Mwalimu safari hii sitaki yatokee kama yaliyopita nataka watoto wote kama wamefaulu waanze shule pamoja Januari hususani kwa watoto wa kike,mtoto wa kike haendi shule miezi miwili ni mingi akiwa kijijini,mtoto wa kiume miezi miwili ni mingi wanaanza shughuli zingine halafu ukimrudisha sekondari ni kazi,kwa hiyo lengo letu hatutaki kujenga madarasa kwa zimamoto,yaani ile mnaanza kukamatana usiende likizo hapana,"amesema.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy ameagiza stendi ya Pongwe iliyojengwa wakati wa Hayati Rais Dkt.John Pombe Magufuli kufunguliwa kabla ya Septemba 15 ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema, uwepo wa stendi hiyo utasaidia kuongeza mapato ya halmashauri, hivyo hategemei kuona inaendelea kukaa bila kutumika na ikiwa tayari asilimia 90 ya mahitaji imeshakamilika.

"Mkurugenzi na kuagiza stendi hii muifungue kabla ya tarehe 15 mwezi huu sioni sababu ya kuendelea kuifunga tunasababisha msongamano wa bure pale kituoni na wakati tayari tumejenga stendi, "alisistiza Waziri Ummy.

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo, Mbaraka Saad alisema atahakikisha anasimamia stendi hiyo iweze kuhudumia wananchi kuanzia sasa.

Diwani Mbaraka alimpongeza waziri Ummy kwa kuchukua hatua ya kutembelea kata hiyo huku akimshukuru kwa namna alivyoweza kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wakazi wa Pongwe wakati wa kampeni zake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news