Afrika yajiandaa kuzalisha chakula cha kutosha

Na Mwandishi Maalum, Addis Ababa

Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika umefunguliwa leo jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine, Mawaziri watapitia Andiko na mikakati ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mwaka 2022 ya “Lishe na Usalama wa Chakula barani Afrika”. 

Kauli mbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa lishe bora kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa watoto barani Afrika, bara ambalo kwa miaka mingi limekuwa linakabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula. 

Hivyo, nchi za Afrika zinashauriwa kutekeleza mapendekezo ya Progarmu ya Afrika ya Maendeleo ya Kilimo na Azimio la Malabo kuhusu kilimo ili kuondokana na changamoto ya lishe duni.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto) na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bi. Eliza Rwitunga wakiwa katika kikao cha kujiandaa na ujumbe wa Tanzania kabla ya kuingia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Afrika. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo na katika mijadala yake, pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika.

Mhe. Mulamula atakumbusha na kulisisitiza suala hilo kwa sababu limeainishwa katika kauli mbiu ya mwaka 2021 ambayo pamoja na mambo mengine, imehimiza matumizi ya lugha za kiafrika na Kiswahili ni moja ya lugha hizo ambayo inakuwa kwa kasi na kuzungumzwa na watu wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akisoma hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa 39 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 14 na 15 Oktoba 2021.

Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo katika hotuba ya ufunguzi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo alisistiza umuhimu wa nchi wanachama kuzingatia tahadhari za maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu wao kupata chanjo ya ugonjwa huo, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha kuwa nchi za Afrika zinapata idadi ya kutosha ya chanjo kwa ajili ya watu wake.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz (kulia) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Caroline Chipeta wakisikiliza hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa 39 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 14 na 15 Oktoba 2021.

Katika Mkutano huo pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje watapitia na kupitisha bajeti ya Mwaka 2022 ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo za makamishna wawili wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Pan Africa, wajumbe wanne wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na wajumbe wanne wa Bodi ya Ushauri ya Afrika ya Kupambana na Rushwa.
Picha ya pmoja ya Mawaziri wa nchi za Umoja wa Afrika wanaoshiriki Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za AU jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Vile vile, Mkutano wa 39 wa Mawaziri utapitia na kupitisha miundo ya taasisi saba za Umoja wa Afrika, ukiwemo muundo wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambalo Tanzania imeridhia Mkataba wake hivi karibuni. Kupitishwa kwa miundo hiyo itakuwa ni fursa zikiwemo za ajira kwa nchi wanachama, hivyo, Balozi Mulamula amewataka Watanzania kuzichangamkia, pindi zitakapotangazwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news