Bumbuli yakamilisha chanjo ya UVIKO-19 Awamu ya Kwanza

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

KAIMU Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga Dkt. Charles Zawagholi amesema zoezi la chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Kwanza limekwenda vizuri kwa wananchi 1,423 kujitokeza kuchanja chanjo, na kuweza kuhitimisha zoezi hilo Oktoba 9, 2021.
Ofisa Afya wa Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga Joyce Mwambashi akitoa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye Gulio la Ijumaa mjini Soni. (Picha na Yusuph Mussa).

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Dkt. Zawagholi alisema walipokea chanjo 2,400, lakini baadae chanjo 600 walizitoa kwa halmashauri nyingine ambayo ilikuwa na uhitaji mkubwa wa chanjo, huku chanjo 377 zikiharibika.

Dkt. Zawagholi alisema wameweza kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi baada ya makundi mbalimbali kwenye jamii kupata elimu ya ugonjwa wa UVIKO 19 na faida ya chanjo yenyewe, ambapo elimu hiyo ilianza kutolewa kwanza kwa wahudumu wa afya, baadae watumishi wa idara mbalimbali ngazi ya halmashauri, na kuwahamasisha baadhi ya viongozi wa Serikali ngazi ya kata, vijiji, viongozi wa dini na wananchi.
Daktari wa Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga Ambwene Mwakyusa akitoa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa mmoja wa wajasiriamali wa mjini Soni Maliwaza Shehoza ambaye ni mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye Gulio la Ijumaa mjini Soni ili kupata chanjo. (Picha na Yusuph Mussa).

"Tulipata chanjo 2,400 , waliochanjwa ni wananchi 1,423 na chanjo zimeisha. Kulikuwa na vituo vya chanjo 24, ambapo hospitali ilikuwa moja, vituo vya afya vitatu na zahanati 20. Lakini pia zoezi hilo limefanikiwa kwa kutoa elimu kwa wasimamizi wa afya ngazi ya halmashauri na watumishi wa idara zote ngazi ya halmashauri ambapo baadhi yao pia walipewa chanjo.
Daktari wa Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga Ambwene Mwakyusa akitoa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa mmoja wa wananchi waliojitokeza kwenye Gulio la Ijumaa mjini Soni. (Picha na Yusuph Mussa).

"Lakini pia tulitoa elimu kwa wahudumu wa afya ikiwemo vituo vya afya, zahanati na hospitali. Pia kulikuwa na baadhi ya madiwani, watendaji wa kata na kuwahamasisha watendaji wa vijiji. Pia watoa Huduma ya Afya kwenye Jamii (CHW) walipata mafunzo ikiwemo viongozi wa dini kwa kuwaita kwenye nakundi na kuwapa elimu, lakini pia kuwafuata waumini kwenye misikitini na kanisani" alisema Dkt. Zawagholi"

Naye Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri ya Bumbuli Elizabeth Nyaki alisema, moja ya changamoto ilikuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na umuhimu wa chanjo yenyewe, kwani elimu bado inahitajika zaidi hasa watakapopokea chanjo ya Awamu ya Pili hivi karibuni.

"Wananchi walikuwa wanaogopa chanjo kutokana na maneno ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa dini kwenye mitandao ya kijamii, namna wanavyoelezea chanjo hiyo, lakini naamini jinsi wananchi watakavyoendelea kupata elimu hiyo wataweza kuchanja kwa wingi, sababu hawa waliochanja Awamu ya Kwanza watakuwa mabalozi wazuri" alisema Nyaki.
Katika kuona zoezi la chanjo ya UVIKO 19 inafanikiwa, Timu ya Uhamasishaji ya Halmashauri ya Bumbuli ikiwa na madaktari, famasia na waratibu akiwemo ofisa mmoja kutoka Mkoa wa Tanga, wakiwa wametinga kwenye Kanisa la KKKT Usharika wa Ngwelo B katika Kijiji cha Msamaka. Mara baada ya kutoa somo, waumini 14 walichanja chanjo hiyo. (Picha na Yusuph Mussa).
Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Bumbuli, Devotha Njalika, akihamasisha kwa kutumia kipaza sauti cha mkononi ili wananchi waliopo kwenye Gulio la Jumamosi la mjini Bumbuli wajitokeze kuchanja chanjo ya UVIKO 19. (Picha na Yusuph Mussa).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news