CAG wa zamani Profesa Mussa Assad afunguka

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Profesa Mussa Assad amefunguka mambo kadhaa ambapo amedai moja ya mambo ambayo yalimuudhi ni jinsi ambavyo aliondolewa madarakani bila utaratibu kufuatwa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mdahalo wa kitabu cha Rai ya Jenerali kilichotungwa na Mwandishi Mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, CAG huyo wa zamani amesema yeye alitolewa ofisini akiwa bado hajamaliza muda wake.

Mdahalo huo ulikuwa umeandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na wasemaji walikuwa ni Jenerali Ulimwengu na Profesa Mussa Assad huku makundi mbalimbali ikiwemo wabunge wakishiriki.

Profesa Assad amesema, kiutaratibu CAG anatakiwa kustaafu akiwa na miaka 60 lakini yeye aliondolewa akiwa bado hajamaliza muda wake kwani leo ndio ametimiza miaka 60.

“Leo ndio siku yangu ya kuzaliwa natimiza miaka 60. Kwa hiyo mara nyingi ukitaja CAG aliyemaliza muda wake huwa silipendi sana kwa sababu kitaalamu nilipotolewa ofisini sikuwa nimemaliza muda wangu na kwa kweli binafsi ni jambo ambalo liliniudhi sana na hatukuwa wazuri katika kusimamia katiba yetu na tumeachia mambo yamekwenda ovyo ovyo,” amesema Profesa Assad.

Amesema kuna haja ya jambo hilo kujadiliwa kwa kina ikiweno Katiba mpya kwani ya sasa imekuwa na baadhi ya mapungufu.

“Katika mazungumzo yetu ya leo haya ni mambo ambayo pia tunatakiwa kuyajadili,” amesema.

Akimzungumzia Jenerali Ulimwengu amesema ni Mwandishi mzuri ambaye amekuwa akisoma Makala zake tangu akiwa Chuo Kikuu.

“Jenerali ni mwandishi mzuri sana nimekuwa nikisoma makala zake enzi hizo nikiwa Chuo Kikuu kila mara kila wakati nilikuwa nasoma magazati yake na ni mtu ambaye ninamtazama kama hazina,”amesema.

Aidha, Profesa Assad amesema kuna watu wamekuwa mazuzu wamesoma sawasawa lakini wanamwogopa mtu mwingine kwa sababu ya kupewa usafiri gairi aina ya V8 pamoja na nyumba nzuri.

“Maana kuna watu wengine sasa hivi wamekuwa mazuzu mtu mzuri amesoma sawasawa lakini anamwogopa mtu mwingine kwa sababu tu labda ile Convort ya V8 ni nzuri kwake au unakaa nyumba ya Serikali kwa sababu anakuwa na wasiwasi akitoka hapo atafanya nini.

“Huko ni kukosa imani kwa sababu wewe kupati rizki yako kwa sababu upo serikalini rizki yako unaipata popote kama ilivyo kwangu ni miaka miwili sasa na mambo alhamdulilah yanaenda vizuri,”amesema Profesa Assad.

Kwa upande wake, Ulimwengu amesema makala hizo ameziandika kuanzia mwaka 1995 lakini ukisoma yale ambayo yapo ndiyo hayo hayo ambayo yanahitajika sasa hivi ikiwemo suala la katiba mpya. Ameongeza kuwa mchakato wa kupatikana katiba mpya bado unahitajika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news