Chanjo ya UVIKO-19 Bumbuli ni nyumba kwa nyumba

Na Yusuph Mussa, Bumbuli

HALMASHAURI ya Wilaya ya Bumbuli mkoani Tanga imeamua kuchanja chanjo ya UVIKO 19 nyumba kwa nyumba na kwenye magulio, masoko , migahawa na hotelii ili kuona zoezi hilo linafanikiwa.
Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Marko Lucas (kulia) akimchanja Nancy Shekifu wa Bumbuli mjini akiwa nyumbani kwake. Halmashauri ya Bumbuli inachanja chanjo ya UVIKO 19 nyumba kwa nyumba. (Picha na Yusuph Mussa).

Wahudumu wa afya ambao wanapita kwa miguu mitaani na kutangaza watu waweze kujitokeza kuchanja chanjo hiyo, baadhi ya maeneo wananchi wamehamasika, na kuomba wapelekewe chanjo hiyo nyumbani kwao badala ya wao kwenda kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 3, 2021, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Dkt. Idd Msuya alisema hawaoni shida kumfuata mwananchi nyumbani kwake ili apate chanjo, kwani wamebaini kwenye maisha kuna changamoto nyingi ikiwemo wengine kushindwa kutembea, aidha kwa ugonjwa ama kwa uzee.
Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Marko Lucas (kulia) akimchanja mmoja wa wazee maarufu mjini Bumbuli ambaye alimfuata nyumbani kwake Alhaji Nurdeen Saleh Hozza (89). Pamoja na kuwa na taaluma ya udaktari wa binadamu, Hozza alikuwa ni mmiliki wa mabasi ya Kampuni ya Katiba na Taifa yaliyokuwa yanafanya safari zake Bumbuli- Tanga na Bumbuli- Dar es Salaam. miaka ya 1970 na 1980. (Picha na Yusuph Mussa).

"Tumeamua kutoa chanjo kwenye masoko na migahawa. Lakini pia tunafanya hivyo kwenye hotelii na nyumba kwa nyumba. Wahudumu wetu wanapita mitaani kwa miguu huku wakiwa na vipaza sauti, na kuwaeleza wananchi umuhimu wa kuchanja. Na kweli wananchi wengi wameanza kuelewa umuhimu wa chanjo, na kuwaita wahudumu wa afya nyumbani kwao ili wawachanje.

"Zoezi hili limeanza kutupa matumaini, kwa wananchi kuanza kujitokeza. Hadi Oktoba 2, 2021 tumechanja wananchi 648, na Oktoba 2, 2021 peke yake tumechanja wananchi 150. Hivyo tunakwenda. vizuri Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli tulipata chanjo 2,400. Nina hakika mpaka zoezi hili litakapofika mwisho tutakuwa tumefanikiwa kwa asilimia 100" alisema Dkt. Msuya.

Katika watu waliofuatwa nyumbani na kuamua kuchanja ni Alhaji Nurdeen Saleh Hozza (89) mkazi wa Kijiji cha Misheni mjini Bumbuli. Pamoja na kuwa na taaluma ya udaktari wa binadamu, yeye alikuwa ni mmiliki wa mabasi ya Kampuni ya Katiba na Taifa yaliyokuwa yanafanya safari zake Bumbuli- Tanga na Bumbuli- Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news