DC Lushoto: Mzazi aliyemtorosha mtoto, atasoma yeye sekondari

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro ameonya kuwa mzazi atakayemtorosha mtoto wake kwenda Mombasa, Kenya kufanya kazi za ndani (House Girl) itabidi yeye ndiyo aende akasome kidato cha kwanza hadi cha nne, tena aweze kufaulu.
Alisema hatakubali kuona Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anajenga vyumba vya madarasa, huku wazazi wanatorosha watoto wao hasa wa kike kwenda kufanya kazi za ndani, na kuagiza kama kuna mzazi ameshafanya hivyo amrudishe mtoto huyo mapema kabla ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba hayajatoka.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara juzi Oktoba 4, 2021 uliofanyika Kijiji cha Kwemakame, Kata Kwai, Lazaro alisema anazo taarifa kuwa kuna watu wameanza kuwapeleka mjini watoto wao wakafanye kazi za ndani, hivyo atachukua hatua na kuona hakuna mwanafunzi atafaulu halafu ashindwe kwenda sekondari.

"Kama mtoto wako amefaulu kwenda sekondari, halafu, wewe ukampeleka Mombasa, Dar es Salaam au Arusha kuwa house girl (mfanyakazi wa ndani) wewe ndiyo utakwenda kukaa darasani kuanza kidato cha kwanza hadi cha nne, na unatakiwa ufaulu. Haiwezekani Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anasomesha watoto wetu bila malipo, lakini bado sisi tunacheza na elimu.

"Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, peke yake kwa mwezi inapokea sh. bilioni moja kwa elimu bila malipo kwa shule za msingi, huku shule za sekondari inapokea sh. milioni 500. Diwani shughulika na wazazi ambao hawataki watoto wao kusoma. Itakuwa ni jambo la ajabu na aibu wewe mzazi kumpeleka mtoto wako Mombasa akamfulie nguo baba mtu mzima au kupiga deki... kaa na mtoto wako umuendeleze kielimu," alisema Lazaro.

Lazaro alisema safari hii hatakubali wilaya yake kuwa ya mwisho kielimu, kwani kwenye matokeo ya mitihani darasa la saba 2020, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ilitoa shule nane (8) za mwisho kitaifa kati ya 10 nchi nzima.

"Mimi siwezi kusutwa mwakani kwa kuwa wa mwisho. Nataka kuhakikisha watoto wote wanafaulu. Na wakati wa kufanyika kwa mitihani, mimi nilipita huko na kukuta watoto wana ari kubwa ya kufanya vizuri, hivyo wazazi tusiwaangushe watoto hawa ili waweze kuendelea na masomo. Maana kuna wazazi huwa wanawaeleza watoto wasifaulu mitihani yao ili wawapeleke mjini kuwa house girl," alisema Lazaro.
Lazaro aliwasifu viongozi na wananchi wa Kata ya Kwai kwa kuweza kujenga maboma mengi ya vituo vya afya, zahanati, madarasa, nyumba za walimu, maabara za sayansi na matundu ya vyoo kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo bila halmashauri ama Serikali Kuu kuchangia, hivyo amewaahidi kuwa Serikali Kuu na halmashauri, watamalizia miradi hiyo.

"Pamoja na kwamba wananchi wa Wilaya ya Lushoto wanajitolea sana kuchangia shughuli za maendeleo, sijawahi kuona kata imejenga vitu vingi kwa njia ya wananchi na Mfuko wa Mbunge kama Kata ya Kwai. Nataka kuwaahidi ifikapo Januari, mwakani itakuwa ni historia kuwa na maboma, kwani tutamalizia maboma ya vituo vya afya, zahanati na shule itakuwa historia,"alisema.

Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi ambaye ziara hiyo ni yake, alisema changamoto za maji na umeme kwenye kata hiyo zitapatiwa ufumbuzi. Lakini pia barabara za kata hiyo, nyingi zipo kwenye mpango wa kufanyiwa matengenezo.

Shekilindi alisema Jimbo la Lushoto limepata sh. bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe. Na barabara ya lami kutoka Lushoto kwenda Mlola ya kilomita 44 imefika Kata ya Migambo, hivyo muda si mrefu itafika Kata ya Kwai, kwani badala ya kujenga kilomita moja kila mwaka, ameomba ijengwe kwa kilomita nne kila mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge 'Makihiyo', alisema vikundi vitatu vya wanawake wajasiriamali kwenye Kata ya Kwai wamepatiwa mkopo wa sh. milioni 11, huku kikundi cha Umoja kikitarajiwa kupata mkopo hivi karibuni. Na kuongeza kuwa changamoto iliyopo ni urejeshaji wa fedha hizo, na kutoa wito waliokopa na kumaliza muda wao waweze kurejesha mkopo huo ili wengine wakopeshwe.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kwai Johari Ndossy alisema maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo ni la zahanati Kijiji cha Kwai, boma la zahanati Kijiji cha Kwemakame ambalo Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi ameomba liwe kituo cha afya na Mkuu wa Wilaya ameridhia kwasababu ya ukubwa na ubora wake.

"Maboma mawili Shule ya Msingi Dindira yote yamepigwa bati na moja lipo hatua ya usafi, nyumba za walimu mbili Shule ya Msingi Dindira yamepigwa bati na upande mwalimu anaishi, boma la maabara tatu Sekondari ya Kijiji Cha kireti, mawili yamepauliwa na moja usawa wa madirisha, maboma matatu ya maabara Shule ya Sekondari Kwai, mawili yamepigwa bati na moja lipo hatua ya lenta, nyumba mbili za walimu Kwai sekondari zimepigwa bati, nyumba mbili za walimu Shule ya Msingi Kwemakame zimepigwa bati na darasa moja Shule ya Msingi Kireti limepigwa bati" alisema Ndossy.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news