Edna Meela, Irene Msengi wampa faraja Dkt.Kikwete mahafali ya UDSM

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kupiga hatua katika usawa wa jinsia hususani kwa wahitimu chuoni hapo mwaka huu wa masomo 2021.
Pongezi hizo amezitoa wakati akiwatunuku vyeti wahitimu wapatao 4,298 wa awamu ya pili katika ngazi ya shahada ya kwanza akisema kuwa amefurahishwa na idadi ya wanafunzi wa kike kuongezeka mwaka hadi mwaka na kuutaka uongozi wa UDSM kuhakikisha usawa wa kijinsia kwa wahitimu unafikia asilimia 50 kwa 50.
Mahafali hayo yamefanyika Oktoba 16,2021 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Kati yao, wanawake ni 1,973 sawa na asilimia 45.9. Dkt.Kikwete ameeleza kufarijika zaidi kuona katika wahitimu wawili, Bi. Edna Meela na Irene Msengi ni miongoni mwa walioongoza kwa GPA kubwa.
Awali Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dkt. William Anangisye amesema kwamba, chuo hicho kimepata mafanikio makumbwa ikiwemo kupata kiasi cha Shilingi Billioni 3 kwa ajili ya kufanya utafiti na ubunifu,pamoja na kuanza kudahili wanafunzi kutoka mataifa ya kigeni kwa ajili ya kujifunza lugha ya Kiswahili.

Profesa Anangisye amewaasa wahitimu hao kuwajibika kwa kutumia elimu zao kuwa na ushawishi wa kuleta chachu ya maendeleo katika Taifa na Dunia kwa ujumla, kufanya kazi kwa bidii, pamoja na kuendelea kujifunza mambo mapya na sio kubaki nyuma.

"Tunawapongeza sana mnaohitimu leo, lakini napenda niwakumbushe msiende kutegemea kuajiriwa serikalini,bali mkawe chachu ya kutengeneza ajira, mfanye kazi kwa bidii, muwe na nidhamu kazini, mjiendeleze kimaarifa, lakini pia mkipata nafasi za kazi za kujitolea mfanye ili mjijengee uzoefu na kujiamini, kwa hiyo msikate tamaa mnapokumbana na changamoto mbalimbali za kazi," amewaasa Profes huyo.

Nae Mwayekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam ( UDSM), Jaji Mstaafu Damian Lubuva ameshukuru hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kujikinga na ugonjwa wa Uviko -19, na kutumia fursa hiyo kusema kuwa chuo kinaendelea kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.

"Nyinyi wahitimu na wale mnaobakia nawaomba muendelee kuchukua tahadhali kama tunavyoelekezwa na wataalamu wa afya kuhusu ugonjwa wa uviko 19, rais amekuwa mstari wa mbele kutukumbusha haya na sisi tuendelee kumuunga mkono," amesema Jaji Mstaafu Lubuva.

Post a Comment

0 Comments