Hatua kwa hatua HOTUBA ya Rais Dkt.Mwinyi wakati akipokea ndege mbili aina ya Airbus

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea rasmi ndege za Serikali ya Tanzania zilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume jijini Zanzibar leo.

Hatua kwa hatua, DIRAMAKINI Blog tunakusogezea hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kama ifuatavyo hapa chini, karibu...


Mabibi Na Mabwana

Assalam Alaykum

Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya hafla hii muhimu ya mapokezi ya ndege hizi mbili za aina Airbus za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) leo tarehe 8 Oktoba, 2021.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akifuatana wasaidizi wake baada ya kumalizika kwa hafla ya sherehe ya mapokezi ya Ndege 2 Mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakati wa mapokezi rasmi zilipowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Niko hapa kupokea ndege hizi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Natoa shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kushirikiana vizuri katika maandalizi ya hafla hii na kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hili muhimu na la kihistoria hapa Zanzibar.

Kwa hakika wananchi wa Zanzibar wana furaha kubwa kuona kwamba, tukio hili la kihistoria la kupokea ndege hizi za Shirika la ATCL mara hii linafanyika hapa Zanzibar. Ndege zilizotangulia zilipokelewa Dar-es- Salaam na nyingine Mwanza.

Bila shaka, uamuzi wa kufanya mapokezi haya Zanzibar, ni kielelezo cha juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wa Taifa hili katika kuendeleza na kulinda fikra, mawazo na falsafa za Waasisi wa Taifa letu katika kuulinda na kudumisha Muungano wetu.

Ndugu Wananchi,

Mapokezi haya ya Ndege hizi mbili za Airbus zilizotengenezwa nchini Canada ni hatua muhimu katika juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano katika kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania ambalo lilianzishwa mwaka 1977. Ni jambo la kujivunia kwa Watanzania kuwa na Shirika la Ndege lililo imara na lenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora kwa abiria wake wote. Ndege 2 za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zikimwagiwa maji kama ishara ya kupata baraka zilipowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, ambapo mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi(hayupo pichani).[Picha na Ikulu] 08/10/2021. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hutuba yake katika hafla ya mapokezi ya Ndege 2 mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibarzilizowasili leo,ambapo Viongozi mbali mbali wa Serikali wamehudhuria akiwepo na Waziri Mkuu wa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Majaliwa Kassim Majaliwa. [Picha na Ikulu] 08/10/2021. 

Shirika letu hivi sasa lina miliki ndege 11 za kisasa. Kati ya hizo ni Bombardier DASH8 Q400 tatu, Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner moja. Kwa ujumla hivi sasa Shirika linamiliki ndege 11. Lengo ni kuwezesha ATCL kuwa na ndege 16 ifikapo mwaka 2023. Mipango ya kuzipata ndege hizo inaendelea. Nawahimiza wananchi na wafanyabiashara kuendelea kutumia ndege zetu kwa huduma za usafiri wa abiria na mizigo yao.

Ndugu Wananchi

Bila ya shaka haya ni mafanikio makubwa tukijuwa kwamba, sekta ya usafirishaji wa anga, majini na nchi kavu ni msingi muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa letu na mataifa yote duniani. Sekta ya usafirishaji ndio msingi mkubwa katika kukuza sekta ya utalii, biashara, viwanda, kilimo, na madini pamoja na kurahisisha shughuli za watu. Vile vile, maendeleo katika usafiri wa anga yana uhusiano mkubwa na ukuaji wa ajira, siyo tu katika viwanja vya ndege, bali pia katika sekta nyengine mbalimbali.

Serikali zetu zote mbili, kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 - 2025, zimeahadi kuiimarisha sekta ya usafiri kwa kujenga miundombinu ya kisasa. Ndio maana kazi kubwa imefanywa katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuviimarisha Viwanja vya ndege, bandari, barabara pamoja na reli zetu.

Ndugu Wananchi,

Kwa upande wa Viwanja vya Ndege, tumeshuhudia mafanikio ya kupigiwa mfano katika kukiimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha Dar es Salaam na Kiwanja hiki cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume. Ni habari njema kuona kwamba, mkataba wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Dodoma umesainiwa tarehe 13 Septemba, 2021.

Hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza mazungumzo na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kukiimarisha zaidi Kiwanja cha Ndege cha Pemba, ili kiende sambamba na dhamira yetu ya kukuza uwekezaji Kisiwani humo pamoja na kukifanya Kisiwa cha Pemba kuwa eneo maalum la Kimkakati la Uwekezaji.

Ndugu Wananchi,

Juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zetu za kukuza sekta ya usafirishaji zina umuhimu wa pekee kwa upande wa Zanzibar katika kukuza sekta ya utalii ambayo ndio muhimili mkuu wa uchumi wetu. Ni matumaini yangu kwamba, uongozi wa ATCL utaendelea kubuni na kupanga mikakati imara ya kibiashara ili kuhakikisha kwamba, malengo ya Serikali zetu ya kuongeza idadi ya ndege kwa ajili ya kukuza uchumi wetu inafanikiwa.

Ni dhahiri kwamba, hivi sasa sekta ya usafiri wa anga imeathirika sana kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa COVID -19, ambao umeathiri sana sekta ya utalii na biashara. Hivi sasa, hali ya uchumi wa dunia inaanza kuimarika na sekta ya usafirishaji inaanza kurejea katika hali ya kawaida. Kwa hivyo, ni jukumu la viongozi waliokabidhiwa kuliendesha Shirika hili la ATCL kuhakikisha kwamba, wanazigeuza changamoto zilizopo kuwa fursa. Wana kazi ya kubuni na kutekeleza mipango mbalimbali itayowezesha kuhimili na kushinda ushindani mkubwa wa masoko uliopo katika sekta ya usafiri wa anga. Shirika lazima liwe mfano katika kutoa huduma bora na kufuata miongozo ya afya inayotolewa hivi sasa na taasisi za Kitaifa na Kimataifa, ili kuwahakikishia usalama abiria wanaotumia ndege zetu.

Ndugu wananchi,

Bado zipo fursa nyingi katika soko la ndani na masoko ya kikanda katika sekta ya usafiri wa anga. Idadi ya Watanzania hivi sasa inakaridiwa kufika milioni 60 au zaidi. Vile vile, shughuli za kiuchumi zinazidi kupanuka na miji yetu inazidi kukua. Hata hivyo bado ni idadi ndogo tu ya Watanzania wanaotumia usafiri wa anga. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisalimiana na Marubani wa Ndege Mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakati wa mapokezi rasmi zilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar leo [Picha na Ikulu] 08/10/2021. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisalimiana na Wahudumu wa Ndege Mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakati wa mapokezi rasmi zilipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar leo [Picha na Ikulu] 08/10/2021. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa mgeni rasmin na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Majaliwa Kassim Majaliwa (katikati) pamoja na Viongozi wengine wakisimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa katika hafla ya sherehe ya mapokezi ya Ndege 2 mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani karume Zanzibar leo [Picha na Ikulu] 08/10/2021.

Ni kazi ya uongozi wa Shirika kuwashajiisha Watanzania kutumia usafiri wa ndege. Nchi yetu ni kubwa tunahitaji huduma za haraka, zilizo salama na za uhakika za usafiri. Bado usafiri wa anga unajulikana kuwa ni usafiri ulio salama zaidi kuliko aina nyengine zote za usafiri. Nafahamu kuwepo kwa changamoto ya gharama lakini kwa kadri watakavyozitumia ndege hizi, basi bei itakuwa inashuka na shirika hili litaendelea kupata faida kubwa zaidi. Tujifunze kwa nchi ambazo zimefanya vizuri katika sekta hii.

Vile vile, ni vyema tukakumbushana kwamba, ufanisi wa ndege hizi kwa hapa petu Tanzania utategemea zaidi juhudi na ufanisi wa huduma zinazotolewa na taasisi zote zilizopo katika Viwanja vya ndege, mfano huduma za uhamiaji, afya, Mamlaka za Kodi n.k kila moja inaweza kuathiri ufanisi wa Taasisi nyengine. Kwa hivyo nazihimiza taasisi zetu zilizopo kwenye viwanja vya ndege kufanya kazi kwa ushirikiano na ufanisi unaotakiwa.

Ndugu wageni walikwa na Ndugu Wananchi,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kulikaribisha Shirika la ATCL katika kuiimarisha sekta ya utalii. Zanzibar inaendelea kuibua masoko mapya ya utalii hasa katika Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali. Juhudi hizi haziendi kwa kasi tunayoitaka kwa sababu bado tunaendelea kutegemea mashirika ya nje yatuletee wageni kutoka maeneo hayo. Naamini kwamba, tukiwa na ndege zenye kufanya safari za moja kwa moja katika viwanja vyetu vilivyo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sekta ya utalii na biashara zitaimarika kwa kasi .

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,

Namalizia hotuba yangu hii, kwa kutoa shukurani zangu za dhati na kuipongeza Kampuni iliyotengeneza ndege hii kutoka Canada kwa kukamilisha vizuri makubaliano yaliyopo.

Aidha, kwa mara nyengine tena, natoa shukurani kwa uongozi wa Wizara Ujenzi na Uchukuzi, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizi. Vile vile, natoa shukurani kwa wasanii wetu, wanahabari, pamoja na wananchi wote waliojumuika nasi katika shughuli hii.

Tunamuomba Mola wetu, audumishe Muungano wetu na aizidishe hali ya amani, umoja na mshikamano iliopo nchini. Nakutakieni nyote kila la kheri na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku. Nataka kuwaambia (ATCL) kwamba nimelipokea ombi lao la kupata ofisi katika sehemu ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume hili tutalifanyia kazi.

Baada ya maelezo haya, sasa napenda nitamke kwamba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ndege mpya za Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) zimepokelewa rasmi.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news