Jeshi la Polisi, wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji mkoani Mara wakubaliana

Na Fresha Kinasa, Mara

Jeshi la Polisi Mkoani Mara limewahakikishia ushirikiano wa dhati wenyeviti wa Serikali za mitaaa na vitongoji katika kuhakikisha wanashirikiana vyema kukabiliana na vitendo vya kihalifu na kwamba, limewaomba wawe wawazi na wakweli kuwafichua wahalifu katika maeneo yao bila kuwaficha.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Ally Kitumbo akizungumza katika kikao cha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Manispaa ya Musoma.Kulia kwake ni Afisa Oparesheni wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, Thomas Mapuli na Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa wa Manispaa ya Musoma, Kizito Manyama.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 21, 2021 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Ally Kitumbo wakati akizungumza na Wenyeviti wa Serikali za mitaaa wa Manispaa ya Musoma katika kikao ambacho kimefanyika katika Kata ya Nyakato. Ambapo kiliandaliwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Musoma, SSP Jumanne Mkwama kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Manispaa ya Musoma kwa lengo la kuwekeana mikakati ya pamoja kumaliza uhalifu ili wananchi waendelee kuishi kwa amani na utulivu.

ACP Kitumbo amesema, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni muhimu sana katika kuimarisha suala la amani na utulivu katika maeneo yao, hivyo amewasisitiza kujitambua vyema na kutumia nafasi yao kuimarisha amani, utulivu na usalama na kwamba, wasiwe chanzo cha kuwaficha waharifu na kufumbia macho vitendo viovu na kuwaachia Jeshi la polisi peke yao kupambana na uhalifu huku wao wanaishi na Wananchi ambao wanatambua tabia zao kwa ukaribu zaidi kwani wanaishi nao

"Polisi tupo tayari muda wote, wakati wowote kushirikiana na Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Wananchi kuhakikisha kwamba uhalifu unakwisha. Niwaombe msisite kuwachukulia hatua watu wachache ambao wanavuruga amani kwa kujihusisha na uhalifu katika maeneo yenu, lengo ni kuona wananchi wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu ni ukweli usiopingika kwamba mnakaa na wananchi kwa hiyo umuhimu wenu ni mkubwa sana katika kumaliza uhalifu tutaendelea kuwapa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kwa ukaribu zaidi,"amesema ACP Kitumbo.

Katika hatua nyingine, ACP Kitumbo amewaomba pia Viongozi hao kutokuwa sehemu ya kudhoofisha ufanisi wa kukabiliana na waharifu ikiwemo kuwapa taarifa mapema waharifu kabla hawajakamatwa na hivyo kutoroka Jambo ambalo amesema wao kama Viongozi hawapaswi kufanya hivyo.

Kwa upande wake Afisa Oparesheni wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, ACP Thomas Mapuli akizungumza katika kikao hicho, amesema Wananchi pia wanapaswa kuendelea kuliamini jeshi la Polisi na kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba utulivu na amani muda wote unakuwepo katika jamii

Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa Manispaa ya Musoma, Kizito Manyama amesema awali ushirikiano na ushirikishwaji ulikuwa hafifu Kati ya uongozi wa Polisi wa Wilaya ya Musoma uliopita na Viongozi hao lakini kwa Sasa amesema wamejenga mahusiano mema ya ushirikiano na pia wamekubaliana kudhibiti uhalifu kwa kufanya doria mtaa kwa mtaa kwa kufanya oparesheni ili kumaliza uhalifu.

Pia, amempongeza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Musoma SSP Jumanne Mkwama baada ya kuripoti katika Wilaya ya Musoma aliomba afanye mkutano huo na Wenyeviti Jambo ambalo amesema ni jema kwani ametambua na kuthamini umuhimu wao katika kuimarisha amani na utulivu na hivyo akaahidi kuendeleza umoja na ushirikiano Kati ya Polisi na Viongozi hao

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Musoma SSP Jumanne Mkwama amesema kupitia kikao hicho cha kutambuana na kuwekeana mikakati ya kumaliza uharifu katika maeneo ya Manispaa ya Musoma. Ameshukuru mwitikio wa Viongozi hao kuhudhuria kikao hicho na amewaomba kuyazingatia yote waliyopangiana kwa maslahi mapana ya Maendeleo ya wakazi wa Manispaa ya Musoma.

Post a Comment

0 Comments