KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE MASUALA YA UKIMWI YATEMBELEA MRADI WA TIMIZA MALENGO IRAMBA SINGIDA

NA MWANDISHI WETU

Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI imefanya ziara ya kukagua utekeleaji wa shughuli za Mradi wa kinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, mradi wa Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) unaotekelezwa katika Wilaya ya Iramba mkoa wa Singida.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akieleza mikakati ya Serikali katika kuhakikisha inatekeleza mipango mbalimbali ili kuendana na malengo ya Dunia kuwa ifikapo 2030 kuhakikisha hakuna maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI. Waziri amesema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI ilipotembelea kuona utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Bw. Kaspar Mmuya na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamai hiyo Mhe. Fatma Taufiq.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Fatma Taufiq (katikati) walipotembelea kuona utekelezaji shughuli za mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na TACAIDS, tarehe 16 Oktoba, 2021 Wilaya ya Iramba Mkoa wa Singida.

Kamati ilitembelea mradi huo tarehe 16 Oktoba, 2021 ili kujionea maendeleo ya mradi huo kwa lengo la kuona namna miradi inayotekelezwa na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

Mradi wa Timiza Malengo unaoratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na kutekelezwa na Serikali kupitia Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine kama TAMISEMI, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknoloji, Taasisi ya Elimu, Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) ,TASAF, AMREF na TAYOA.

Mradi huo umetekelezwa kwa muda wa miaka 3 tangu Januari 2018 hadi Disemba 2020 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na walengwa wakiwa wasichana balehe na wanawake vijana waliopo kwenye vijiji 50 vinavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Wilayani humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI Mhe. Fatma Taufiq akizungumza kuhusu masuala ya kuzingatia kwa wanufaika wa mradi wa Timiza Malengo wakati wa mkutano wao na wadau hao.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI wakifuatilia kikao hicho.

Hadi sasa mradi umeifikia mikoa mitano ya mfano ikiwemo; Morogoro, Dodoma, Singida, Geita na Tanga ambapo wamelenga kundi la wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 walio ndani ya mfumo wa shule, kuendelea na masomo na kufikia ndoto zao wakiwa salama bila maambukizi ya VVU/ UKIMWI.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatma Taufiq akizungumza wakati wa kikao cha ufunguzi alisema ni muhimu kwa Serikali kuendelea kutoa elimu na kuyafikia makundi ya wasichana balehe kwa kuzingatia ndilo kundi lililo katika hatari ya kupata maambukuzi ya VVU huku akiwaasa vijana kuitumia miradi hiyo kama chachu kujikwamua kiuchumia na kutimiza ndoto zao huku wakichangia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Tumetembeela kuona jinsi Serikali inavyotekeleza afua mbalimbali ili kuhakikisha kundi la vijana linalotajwa kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU na UKIMIMWI yanahudumiwa ipasavyo na kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya”

Aliongezea kuwa, miradi hiyo inapaswa kufanyika kwa usahihi ili kuwa na tija katika jamii zetu na kuhakikisha inakuwekewa mipango endelevu na kuifikia mikoa yote ili kuwa na vijana wenye kujitambua na kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akieleza namna mkoa wake unavyounga mkono jitihada za kutokomeza maambukizi mapyaya Virusi vya UKIMWI kwa vijana wakati wa kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI katika ofisi yake mkoni humo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Mwenda akieleza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI kabla ya kutembelea miradi ya Timiza Malengo inayoratibiwa Wilayani hapo mkoa wa Singida.

Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inawafikia wasichana balehe na wanawake vijana kwa wingi kwa kuhakikisa mradi huu wa Timiza Malengo unafika katika mikoa yote nchini.

“Mradi huu umeanza katika mikoa hii mitano ya mfano, ni malengo kuwafikia vijana wetu wa Kitanzania ili waweze kupatia elimu itakayowasaidia kujitambua na kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwapekelea katika maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,”Alisema Waziri Mhagama

Aliongezea kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha jamii inabadili mitazamo kuhusu kundi hili la wasichana balehe na wanawake vijana ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili wajikwamue na kuinua wengine.

Aidha aliwaelekeza watendaji wa Wilaya ya hiyo kuhakikisha wanakuwa na kanzi data ya wanufaika hao, kusaidia uendelevu wa programu na kuhakikisha waelimisha rika wanapatiwa ushirikiano wa kutosha ili wafikie kundi kubwa lililoachwa nyuma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI Mhe. Fatma Taufiq akikabidhi mchango wa kuwasaidia wanufaika wa mradi wa Timiza Malengo Bi. Jamila Hassan (mwenye ushungi) na Mariam Juma (mwenye blauzi nyekundu) walioweza kujiendelea katika shughuli za uzalishaji za uuzaji mafuta ya kupikia na vitunguu na kuweza kujenga nyumba za makazi Wilayani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiendesha harambee ya kuwawezesha kununua mabati wanafuaika wa mradi huo Bi. Jamila Hassan an Mariam Juma ambao wanalea familia zao mara baada ya wazazi wao kufariki kwa ajali ya gari katika kijiji cha Maluga Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Mmoja wa wanufaika wa mradi nje ya mfumo wa shule Bi. Neema Naaman akionesha kuku wa nyama aliofuga kutokana na uwezeshwaji wa mtaji kutoka mradi wa Timiza Malengo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Masuala ya UKIMWI katika Wilaya ya Iramba Singida.
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Lulumba, Maria Hamis (mnufaika) akieleza mafanikio ya uwepo wa mradi wa Timiza Malengo ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu wao shuleni wakati wa kikoa cha Kamati ya Kudumu ya Bunge UKIMWI walipotembelea kuona utekelezaji wake. (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).

“Serikali imelilenga kundi hilo kwa kuzingatia takwimu za mwaka 2017 ambapo zinaeleza vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 40 ya maambukizi mapya na kati yao asilimia 80 ni watoto wetu wa kike, hii ni dalili kwamba lazima mapambano haya yazidishwe katika makundi haya hatarishi”alisema Waziri Mhagama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Suleiman Mwenda aliishukuru kamati hiyo kutembelea na kuona utekelezaji wa programu ya TIimiza Malengo na kuendelea kuahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maeneo yote muhimu yanayohusu mradi yanaendelea vyema huku akimshukuru Waziri Mhagama kwa kutoa kipaumbele kwa wilaya hiyo na kusema wataendelea kutunza kanzi data ya wanufaika wa mradi ili matunda yanayotokana na mradi huo yasipoteee.

“Wilaya itaendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha kunakuwa na bajeti ya kutosha katika kuyahudumia makubdi haya muhimu kwenye jamii,”alisema Mwenda.

Wakitoa shukrani na shuhuda zao tangu kuanza kwa mradi huo wanafunzi wa shule za sekondari za Lulumba na New Kiomboi waliishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo huku wakisema umewawezesha kuongeza hali ya ufaulu, kujikimu kiuchumi na kupata mahitaji yao kwa wakati na kuwasaidia familia zao katika mahitaji mbalimbali.

AWALI

Mradi wa timiza Malengo unahusisha ugawaji wa taulo za kike kwa wasichana walio ndani ya mfumo wa shule, kugawa kondom na kufunga visanduku vya kondom katika maeneo husika, kutoa elimu kwa viongozi wa dini kuhusu masuala ya UKIMWI, Utoaji wa mafunzo kuhusu uandaji wa mpango rahisi wa biashara na ujasiriamali, elimu ya malezi na makuzi kwa wazazi au walezi wa wasichana, kuhamasisha wasichana kupima afya zao kwa hiari kupitia huduma ya mkoba na Vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao kupitia mabonanza, kuwawezesha wasichana kwa kuwapatia ujuzi wa jinsi ya kujikinga na maambukizi pamoja na kutoa elimu kwa njia ya simu kwa kupitia namba 117/15017- bure ambapo wanapokea na kupata fursa ya kuuliza maswali na kupatiwa majibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news