Kanisa la Mchungaji Nick Shaboka na Rose Shaboka la 'New Day Church International' lakabiliwa na upinzani Kinondoni, watoa waraka mzito, wahusika wakuu majina yao yawekwa hadharani



UKANDAMIZWAJI WA KANISA

Kanisa la Tanzania na wote wenye mapenzi mema tuombe kwa ajili ya ndugu zetu wa kanisa la NEW DAY CHURCH INTERNATIONAL - (MADHABAHU YA MOTO) maana wanapitia adha na upinzani mkubwa unaoratibiwa na Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Bunju A na baadhi ya Watendaji wa Manispaa kutoka Wilaya ya Konondoni.

Tangu kanisa lihamie eneo hilo ambalo kwa miaka zaidi ya 10 lilikua linatumika kama Bar na ukumbi wa maharusi uliokua unajulikana kama ukumbi wa VALENTINO, kumekuwa na usumbufu mkubwa na vitisho vingi.

Usumbufu huu unasababishwa na jirani mmoja tu ambaye katika vikao vyote vilivyofanyika kati yake na uongozi wa kanisa alikua akidanganya jina na kutumia jina la Mama yake aitwaye LILLIAN MAGOTI ambaye pia anaishi eneo hilo.

Tangu siku ya kwanza kanisa linapita kuwataarifu majirani kuhusu kutumia ukumbi huo kwa matumizi ya Ibada na kuwakaribisha, jirani huyo ALIAPA kwamba kanisa halitakaa mahali hapo kwa sababu yeye HAPENDI NA HATAKI MAOMBI eneo hilo.

Ikumbukwe kiwanja sio cha jirani huyo ila yeye ni jirani tu na kanisa halijavamia eneo na wala kanisa halina mgogoro wowote na mmiliki wa eneo. Na eneo hili limetumika kama bar na ukumbi kwa miaka mingi na miziki ilikua inapigwa sana na hakuna aliyewahi kulalamika popote.

Zaidi ya mara tatu uongozi wa kanisa umeomba kikao na majirani pamoja na viongozi wa serikali za mitaa lakini kikao hicho kilishindikana kwa sababu hakuna jirani aliyejitokeza kuipinga kazi ya Mungu eneo hilo isipokua jirani huyo mmoja ambaye katika vikao vyote alikua akidanganya jina kwa kutumia jina la Mama yake aitwaye LILLIAN MAGOTI huku akidai kwamba majirani wengine wamemtuma yeye.

Katika moja ya vikao aliwasilisha saini alizodai ni majirani wengine walisaini kusema kwamba hawataki kanisa eneo hilo lakini tulipofuatilia tuligundua saini nyingine ni FEKI na majirani ambao walionyesha kuwa upande wa kanisa hawakusaini wala kuhusishwa.

Jirani huyu alienda mbali zaidi kwa kumvamia Mchungaji ibadani na kuanza kugombana nae mbele ya washirika. Zaidi ya hayo alileta matarumbeta na vigodoro na vikawa vinapigwa muda wa ibada na kusababisha kelele mtaa mzima ili ibada zisiendelee kwa utulivu huku akijitapa kwamba ataendea mpaka tuhame.

Haikutosha, akawatukana Watumishi wa Mungu walipokua katika ibada ya live kupitia mtandao wa Instagram kwa page yake ya biashara ya @zamartanzania akiwaita MATAPELI.

Haikuishia hapo, akaendelea kutishia kwamba ana uwezo wa kupiga simu moja tu na kanisa likafungwa na inaonekana ana mahusiano ya kindugu au kirafiki na viongozi wakubwa serikani ambao muda ukifika tutawataja hadharani.

Jirani huyu amekua akipitapita pia eneo la kanisa akichukua video na picha kwa simu yake na hatujui anakozipeleka. Na kwa waraka huu tunafahamu kwamba utamfikia hivyo tunamuonya asirudie kuchukua picha na video eneo hilo kwa sababu tutamchukulia hatua kali.

Jirani huyu akishirikiana na Mtendaji wa Mtaa wa Mbezi A Bwana Said Kikuyu na baadhi ya watendaji wa Manispaa akiwemo Bwana Mugi waliamua kulipeleka kanisa Mahakamani kwa kesi ya KELELE baada ya kuona jitihada zote za kuzuia ibada zinashindikana.

Tulipowaambia watupe muda tutaweka sound proof kutatua shida ya kelele walitukebehi kwamba HATUNA UWEZO HUO. Na hata tulipoanza na wakaona tunaweza waliweka mkakati wa kubadilisha CHARGES mahakamani isiwe KELELE tena ila iwe ni MAJIRANI HAWATAKI KANISA eneo hilo ambapo siku ya kutoa ushahidi mahakamani hakuna jirani aliyefika zaidi ya jirani huyo anayetumia jina la LILLIAN MAGOTI na kesi hiyo kuahirishwa.

Kesi ikiwa inaendelea mahakamani na kwa kuona umuhimu wa kutatua shida ya kelele iliyokua inalalamikiwa na jirani yetu LILLIAN MAGOTI kwa haraka, pamoja na changamoto zingine tulizozikuta kwenye ukumbi ikiwemo kuvuja wakati wa mvua kwa sababu ulikua ukumbi wa makuti, na ulijengwa kwa mirunda ambayo ilikua imeanza kuoza kwa sababu imekaa muda mrefu na isingekua salama kwa washirika wanaokuja kuabudu hapo, uongozi wa kanisa ukaamua kutafuta kibali cha kufanya MABORESHO ya ukumbi husika ili pia kuweka SOUND PROOF ili jirani yetu asisikie maombi yetu kama alivyosema.

Tarehe 16/8/2021 Uongozi wa kanisa ukapeleka maombi ya kibali Cha maboresho ya ukumbi katika ofisi za Manispaa ya Kinondoni lakini cha kushangaza barua hiyo IKAZUIWA na KUFICHWA na mtumishi mmoja katika ofisi ya Afisa mipango miji anayeitwa Bwana Mathayo. Lakini pia file la maombi yetu likaandikwa OPEN SPACE wakati sio OPEN SPACE na ni kiwanja halali chenye hati.

Kwa sababu ya DEMAND iliyokuwepo ya washirika kukaa mahali salama na kuzuia kelele zilizokua zinalalamikiwa na jirani, wakati tunasubiri kibali cha maboresho kutoka manispaa tulianza maboresho polepole huku tukiamini Watendaji wetu wa Manispaa wanatambua uharaka na uhitaji tulionao na kibali kitatolewa.

Lakini hatukupewa kibali hicho pamoja na kujaribu kufuatilia sana mpaka tulipogundua mwezi huu wa kumi kwamba barua yetu ILIFICHWA. Tulipouliza kwa nini hatupewi kibali na kwa nini barua ifichwe tukaambiwa eneo lina mgogoro wa majirani na ni eneo la makazi hivyo tuombe eneo la kuweka kanisa MABWEPANDE, tutoe kanisa eneo hilo la Mbezi Beach, wakimaanisha kuwa hata tusihangaike kubadilisha matumizi ya eneo kwa sababu wao hawalitaki kanisa eneo hilo, wanachotaka ni sisi tuhame. Kumbuka kwenye eneo hilohilo la makazi kuna kanisa katoliki na msikiti lakini pia kuna bar kama Juliana na Beach Kidimbwi. Kwa nini sisi tufukuzwe na tuambiwe tuende Mabwepande?.

Wakati maboresho yanaendelea ndipo mkandarasi wa wilaya aitwaye Bwana Dewji akafika kwenye eneo la ukumbi na kuzuia maboresho yasiendelee bila kutoa notice wala barua yoyote.

Wiki hii siku ya Jumatatu saa 12 jioni kwa mara ya pili tena mkandarasi huyohuyo akaja eneo la kanisa akiwa ameongozana na Mtendaji Bwana Saidi Kikuyu pamoja na Afisa mazingira tunaemfahamu kwa jina la Bwana Mugi pamoja na mjumbe wa nyumba kumi aitwaye Bwana Nasor pamoja na MABAUNSA.

Kwa bahati nzuri wakamkuta Mchungaji Kiongozi @apostle_nick_shaboka kanisani na alipowaomba na kuwakaribisha kuingia ofisini walikataa na kuanza kufoka hadharani bila kuistahi heshima ya Kiongozi wa dini na wakaanza kuandika maandishi mengine kwenye ukuta wa kanisa kwamba kila kitu kisimame mara moja.

Mpaka leo bado tunajiuliza kwa nini tulivamiwa saa 12 jioni muda ambao hata ofisi za Serikali zimeshafungwa tena na mabaunsa kama vile sisi ni wezi au wauza madawa ya kulevya au watu wanaofanya jambo baya na hatuna majibu.

Haya yote waliyafanya bila kutoa notice ya barua na tukio zima lilirekodiwa ingawa hawakutaka tufanye hivyo na mabaunsa waliokuja nao walikua wakitoa vitisho na kutaka kunyang'anya kamera huku wengine wakijificha wasichukuliwe na kamera.

Leo asubuhi tarehe 22/10/2021 wamefikisha barua ya notice ya zuio la kuendelea na maboresho ya eneo ambayo wameiandika tarehe za nyuma kabisa na hatujajua wamefanya hivyo kwa makusudi gani na kwa maslahi ya nani?.

Ikumbukwe kuwa hii Mbezi Beach tuliyopo kuna bar nyingi maarufu kama Beach Kidimbwi, Juliana, pamoja na Misikiti na Makanisa mengine mbalimbali ambayo pia yanatumia vipaza sauti na spika ili kuendesha shughuli zao na vyote viko kwenye makazi ya watu lakini kanisa hili la NEW DAY CHURCH INTERNATIONAL ambalo liko jirani na mtu ambaye ana mahusiano ya kindugu au kirafiki na vigogo wa serikalini linapata usumbufu mkubwa na anatumia nafasi hiyo kujaribu kukandamiza kanisa.

Tumejaribu kufikisha swala letu kwa Mkurugenzi lakini tuliambiwa yuko likizo. Tukaenda kwa mkuu wa wilaya ya Konondoni bila kupata ufumbuzi. Lakini pia tukafanya juhudi ya kumtafuta mkuu wa mkoa Dar es salaam Mh Amos Makala kupitia Katibu wake ili tuweze kumuona lakini Katibu alipokea simu mara moja tu, tukamueleza swala letu na akaomba tumpigie siku inayofuata lakini baada ya hapo amekuwa hapokei simu tena na juhudi za kumuona Mkuu wa Mkoa hazijafanikiwa.

Tunayaweka mambo haya hadharani baada ya kujaribu kutafuta suluhu kimyakimya kwa muda mrefu kwa sababu zifuatazo:

1)Kanisa ni taasisi ya watu na inahudumia jamii na ni chombo cha amani na tumejaribu kukaa mezani kujaribu kutafuta suluhu kwa amani bila mafanikio na badala yake tumeendelea kukandamizwa kwa sababu tu ya jirani anayejuana na vigogo ambaye hataki watu waabudu. Kuna siku moja tuliitwa kikao pale wilayani kati ya Uongozi wa kanisa, Uongozi wa mtaa, jirani na Uongozi wa manispaa lakini cha kushangaza jirani yetu na viongozi wa mtaa waliambiwa wafike lisaa limoja kabla ya muda tulioambiwa sisi na tulipofika tukakuta kuna kikao kingine wamemaliza kabla ya kile cha wote. Hii yote inaonyesha yapo mambo yameendelea kufanyika chinichini ili kuvuruga kazi ya Mungu

2)Kanisa sio ADUI wa jamii na majirani wanaolizunguka.

3)Kanisa linapokuwepo eneo husika kuna SPIRITUAL, SOCIAL& ECONOMICAL BENEFITS ambazo wakazi wa eneo husika wanazipata

4)Kanisa halipo kuvunja sheria na liko tayari kuelekezwa na watendaji wa serikali pale linapokua limejisahau au halifahamu taratibu husika bila kutumia VITA, MABAVU na UKANDAMIZAJI

5)Sisi ni VIONGOZI WA WATU na kanisa tunaloliongoza sio PHYSICAL CHURCH tu ila tuna maelfu ya washirika tunaowahudumia MTANDAONI pia na watu hawa ndio wanaotoa sadaka zinazoendesha shughuli zote za kanisa ikiwemo maboresho yaliyokua yanaendelea na tunawajibika kutoa taarifa kwao ya kinachoendelea.

6)Eneo lililokua Bar na leo ni kanisa linalohudumia jamii na kuisaidia serikali kutengeneza jamii na wananchi wema ni jambo la baraka na faida.

7)Tumeyaweka Mambo haya hadharani ili kanisa la TANZANIA na watu wote wenye uchungu na kazi ya Mungu tuombe pamoja lakini pia Watendaji wakuu Serikalini ambao tunaamini WANASIMAMIA HAKI waliangalie jambo hili kwa makini maana huu ni uonevu wa wazi wazi.

NOTE: Hatuandiki haya KUTAFUTA HURUMA YA MTU, ila tunatoa TAARIFA kwa kanisa letu la MTANDAONI na wale wote wanaoifurahia na kuitakia mema kazi tunayoifanya ili wajue juu ya yale yanayoendelea kwa sababu sadaka zao ndizo zinazoendesha kazi hii.

TUMUOMBE MUNGU SANA KWA AJILI YA KANISA LA TANZANIA.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Kazi iendelee.!

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news