Katibu Mkuu CWT: Serikali itenge bajeti kuwaendeleza walimu nchini

Na Robert Kalokola,Geita

Chama Cha walimu Tanzania (CWT) kimeiomba Serikali kutenga bajeti ya kuunga juhudi za mradi wa kujengea uwezo walimu nchini katika masomo ya Kiingereza na Sayansi ulioanzishwa na chama hicho na Shirika la Kimataifa la International Education katika mikoa sita ambao umeonyesha matokeo chanya.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzaniaa Deus Seif (Picha na Robert Kalokola).
Mikoa ambayo imenufaika na mradi huo wa kuendeleza walimu wa sayansi ili waweze kukabiliana na upungufu wa walimu wa Sayansi shuleni ni pamoja na Mkoa wa Arusha,Manyara,Kilimanjaro,Singida,Dodoma na Shinyanga na kwa sasa CWT inaongeza katika awamu ya tatu ya mpango huo inaongeza mikoa ya Lindi na Geita.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa CWT Taifa  Deus Seif katika maadhimisho ya siku ya Mwalimu Duniani wilayani Bukombe ambayo yaliratibiwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko kwa ajili ya kukutana na walimu wote wa wilaya hiyo.

Katibu Mkuu Deus Seif ameeleza kuwa, chama hicho kinaendesha mpango huo ikiwa ni moja ya mbinu ya kukabiliana na upungufu wa walimu wa sayansi nchini ambao hadi sasa umeshatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano na zaidi ya Bilioni 2 zimeshatumika kutekeleza mpango huo.

Ameeleza kuwa, jukumu la kuendeleza walimu kitaaluma ni la serikali hivyo anaishauri kutengwa bajeti kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya pamaoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa Mitaa (Tamisemi) ili kuwezesha walimu hao hata kwa kuanza na mikoa michache ili kuweza kupambana na upungufu uliopo.

Deus Seif amefafanua kuwa, mpango huo umeonyesha matokeo chanya hasa katika mkoa wa Arusha na umechangia kwa kiwango kikubwa Jiji la Arusha kuongoza katika matokeo ya kitaifa kwa kushika nafasi ya pili kutokana na na mafunzo hayo yaliyotolewa kwa walimu wa Sayansi ikiwa ni pamoja na kuandaa zana za kufundishia.

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, ameandaa maadhimisho hayo katika jimbo lake ili iwe sehemu ya kutambua mchango wa walimu katika maisha yake binafsi ,jimbo na Wilaya ya Bukombe na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa maazimio ya Shirika la Kazi Duniani na Shirika la Elimu Dunia kupitisha siku hiyo kuwa ya Mwalimu Duniani itumike na kila mtu kukumbuka na kutambua mchango wa mwalimu wake katika maisha yake ulivyomgusa.

Waziri Dkt.Biteko ametumia siku hiyo ya mwalimu Duniani kutoa zawadi maalum kwa walimu wake watano ambao alisema walitoa mchango wa peke katika maisha yake ambao wote ni walimu wastaafu na kwa sasa wanaishi maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Profesa Kitila Nkumbo amesema kuwa tatizo la upungufu wa walimu ni la nchi nzima, lakini serikali inaendelea kutoa ajira kila mwaka.
Ameongeza kuwa, sekta ya elimu ni moja ya kada zinazo pewa kipaumbele na serikali katika kutoa ajira hivyo ajira zinaendelea kutolewa kulingana na uwezo wa kiuchumi na kadri inavyojenga uwezo wa kifedha.

Senyamule amewataka maafisa Utumishi kuhakikisha wanarekebisha mishahara ya walimu wote kwa kutuma taarifa zao kwa usahihi kwa wale wote wenye sifa za kustahili kupanda ili walimu waweze kufundusha kwa raha.

Akifafanua kuhusu upungufu wa walimu wa Sayansi  Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bukombe, Philbert Nyangahondi amesema kuwa katika wilaya hiyo ina shule za Sekonadari 17 za serikali na tatu za binafsi lakini ina walimu wa Sayansi 87 tu na mahitaji ikiwa nia walimu 252 wa masomo ya Fizikia ,Kemia na Bailojia.

Amesema kuwa, upungufu ni mkubwa hivyo mbinu inayotumika kukabiliana na tatizo hilo ni kutumia walimu wasio rasmi ambao hawajaajiriwa, lakini wamehitimu shahada na stashahada katika masomo ya sayansi.

Ameeleza kuwa, walimu wanaochukuliwa kufundisha masomo hayo ya sayaqnsi ili kuziba pengo hilo wanaondoka kwenye shule hizo kwa kuacha kazi kutokana na kukosa malipo kwa sababu fedha za kuwalipa zinachangwa na wazazi na nyingine kutokana na fedha za fidia ya elimu bure shuleni.
Baadhi ya walimu wamesema kuwa, wanapata chanagamoto kubwa kufundisha masomo ya sayansi kutokana na wingi wa wanafunzi na uchache wa walimu wa sayansi katika shule zao na kulazimika kufundisha vipindi vingi.

Mwalimu Sara Ndegeulaya na Mwalimu Ngwala Josephat kutoka shule ya sekondari Runzewe wanasema wana wanafunzi wengi na wanalazimika kufundisha wanafunzi kwa muda wa ziada ili waweze kumaliza vipindi vyote kwasababu ni wachache katika shule yao.

Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu uadhimishwa kila mwaka Oktoba 5 Duniani Kote kufuatia azimio la Shirika la Kazi Duniani na Shirika la Elimu Duniani mwaka 1966 ikiwa ni kukumbuka umuhimu na mchango wa mwalimu wa kila siku.

Post a Comment

0 Comments