KOROGWE DC YAPOKEA CHANJO YA UVIKO-19 AINA SINOPHARM DOZI 5,000

Na Yusuph Mussa, Korogwe

HALMASHAURI ya Wilaya ya Korogwe (DC) mkoani Tanga imepokea chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm kutoka nchini China dozi 5,000 ambazo zitaweza kuchanja watu 2,500 ikiwa ni chanjo Awamu ya Pili.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Oktoba 22, 2021, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Dkt. Miriam Cheche, alisema chanjo hiyo wamepata Oktoba 21, 2021.

"Tumepokea chanjo ya UVIKO 19 aina ya Sinopharm dozi 5,000. Dozi hizi 5,000 zinaweza kuwachanja takribani watu 2500, kwani hutolewa mara mbili ili kukamilisha dozi kamili na kuimarisha kinga dhidi ya homa kali itokanayo na Virusi vya UVIKO-19. Usambazaji wa chanjo hizo kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma utaanza Oktoba 23, 2021" alisema Dkt. Cheche.

Dkt. Cheche amesema wamejiandaa na chanjo Awamu ya Pili, kwani safari hii hawatatoa mafunzo tena kwa viongozi wa kada mbalimbali, bali watatangaza tu kwa kuwakusanya wananchi kwenye vituo vya afya kama sehemu ya kuwahamasisha waweze kwenda kuchanja, na ikibidi watakuwa kwenye mikutano ya hadhara.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Dkt. Miriam Cheche akitoa chanjo kwa mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Korogwe. Ni chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Kwanza.

"Kwa mafunzo tuliyotoa kwa viongozi wa kada na fani mbalimbali, inatuhakikishia kuwa chanjo ya Awamu ya Pili itafanya zoezi letu kuwa jepesi katika kuchanja, sababu tumeshirikisha wengi. Tulitoa mafunzo kwa viongozi wa CCM kuanzia Kamati ya Siasa ya Wilaya. Kamati hii ina wajumbe 12, lakini walihudhuria tisa, wajumbe wa Sekretarieti ya Wilaya watano na viongozi wa CCM ngazi ya kata 87.

"Lakini pia tulitoa elimu na chanjo Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Lutindi. Tuliona tusiwatenge, kwani ni sehemu ya jamii yetu. Pia tulikwenda Magereza ya ya Kerenge, ambako huko nako tulitoa elimu na kuchanja chanjo ya UVIKO 19, hivyo tunaamini chanjo ya Awamu ya Pili tutatumia matangazo tu kuanzia kwenye magari, na kuwahamasisha wananchi kwenda kuchanja kwenye vituo husika, na kama pia kutakuwa na maeneo ya mikutano yaliyotengwa kwa ajili ya chanjo ili kuhamasisha, tutakwenda huko" alisema Dkt. Cheche.

Dkt. Cheche alisema zoezi la chanjo Awamu ya Kwanza limekwenda vizuri kwa watu 2,202 kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19 na kuweza kuhitimisha zoezi hilo Oktoba 13, 2021. Walipokea chanjo 3,000, lakini kutokana na sababu za kitabibu waliweza kuchanja wananchi 2,202, huku chanjo 798 zikiharibika.

Alisema wameweza kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi baada ya makundi mbalimbali kwenye jamii kupata elimu ya ugonjwa wa UVIKO 19 na faida ya chanjo yenyewe, ambapo elimu hiyo ilianza kutolewa kwanza kwa Kamati ya Afya ya Wilaya (PHC) ikishirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama, wahudumu wa afya, baadae watumishi wa idara mbalimbali ngazi ya halmashauri, viongozi wa Serikali ngazi ya kata, vijiji, viongozi wa dini na wananchi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Dkt. Miriam Cheche (kushoto) akitoa chanjo kwa mmoja wa wananchi wa jamii ya kifugaji katika Kijiji cha Makayo, Kata ya Mkalamo kwenye zoezi la chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Kwanza.

"Tulipata chanjo 3,000 katika Awamu ya Kwanza, waliochanja ni wananchi 2,202 na chanjo zimeisha. Kulikuwa na vituo vya chanjo 53, ambapo hospitali ilikuwa moja, vituo vya afya vitano na zahanati 47. Lakini pia zoezi hilo limefanikiwa kwa kutoa elimu kwa wasimamizi wa afya ngazi ya halmashauri na watumishi wa idara zote ngazi ya halmashauri.

"Lakini pia tulitoa elimu kwa wahudumu wa afya ikiwemo vituo vya afya, zahanati na hospitali. Pia kulikuwa na madiwani, wote kwenye kata 29 na wale wa Viti Maalumu, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji wote. Ofisa Maendeleo Kata na Ofisa Elimu Kata (WEO). Pia Wenyeviti wote wa vijiji 122, watoa Huduma ya Afya kwenye Jamii (CHW) na wananchi" alisema Dkt. Cheche.

Dkt. Cheche alisema moja ya changamoto ilikuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na umuhimu wa chanjo yenyewe, kwani baadhi ya viongozi wa vijiji ambao walikuwa sehemu ya watu waliopata mafunzo, walihoji uhalali wa chanjo hiyo, na walipopata elimu, wao walikuwa wa kwanza kuchanja, hivyo kwa kiasi kikubwa elimu imewafikia wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news