Korogwe yakamilisha chanjo ya UVIKO-19 Awamu ya Kwanza

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Miriam Cheche amesema zoezi la chanjo Awamu ya Kwanza limekwenda vizuri kwa watu 2,202 kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19 na kuweza kuhitimisha zoezi hilo Oktoba 13, 2021.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Cheche alisema walipokea chanjo 3,000, lakini kutokana na sababu za kitabibu waliweza kuchanja wananchi 2,202, huku chanjo 798 zikiharibika.

Alisema wameweza kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi baada ya makundi mbalimbali kwenye jamii kupata elimu ya ugonjwa wa UVIKO 19 na faida ya chanjo yenyewe, ambapo elimu hiyo ilianza kutolewa kwanza kwa Kamati ya Afya ya Wilaya (PHC) ikishirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama, wahudumu wa afya, baadae watumishi wa idara mbalimbali ngazi ya halmashauri, viongozi wa Serikali ngazi ya kata, vijiji, viongozi wa dini na wananchi.

"Tulipata chanjo 3,000, waliochanjwa ni wananchi 2,202 na chanjo zimeisha. Kulikuwa na vituo vya chanjo 53, ambapo hospitali ilikuwa moja, vituo vya afya vitano na zahanati 47. Lakini pia zoezi hilo limefanikiwa kwa kutoa elimu kwa wasimamizi wa afya ngazi ya halmashauri na watumishi wa idara zote ngazi ya halmashauri.

"Lakini pia tulitoa elimu kwa wahudumu wa afya ikiwemo vituo vya afya, zahanati na hospitali. Pia kulikuwa na madiwani, wote kwenye kata 29 na wale wa Viti Maalumu, watendaji wa kata na watendaji wa vijiji wote. Ofisa Maendeleo Kata na Ofisa Elimu Kata (WEO). Pia Wenyeviti wote wa vijiji 122, watoa Huduma ya Afya kwenye Jamii (CHW) na wananchi," alisema Cheche.

Cheche alisema moja ya changamoto ilikuwa ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19 na umuhimu wa chanjo yenyewe, kwani baadhi ya viongozi wa vijiji ambao walikuwa sehemu ya watu waliopata mafunzo, walihoji uhalali wa chanjo hiyo, na walipopata elimu, wao walikuwa wa kwanza kuchanja, hivyo kwa kiasi kikubwa elimu imewafikia wananchi, lakini bado elimu inahitajika zaidi hasa watakapopokea chanjo ya Awamu ya Pili hivi karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news