Maagizo ya Waziri Rahma Kassim Ali kwa UCSAF, asisitiza wenye ulemavu wasiachwe nyuma

Na Doreen Aloyce, Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Rahma Kassim Ali ametoa wito kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF) kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele kwenye mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili waweze kunufaika na huduma hiyo.

Ameyasema hayo jijini Dodoma alipotembelea ofisi za UCSAF ambapo amesisitiza huduma za mawasiliano hazipaswi kuwaacha nyuma watu wenye ulemavu, kwani nao wana haki ya kunufaika na huduma hizo.

"Tunapoenda mbele zaidi katika mawasiliano hatupaswi kuwaacha wenzetu hawa watu wenye ulemavu kwani wakipatiwa mafunzo watakuwa na uelewa zaidi,"amesema Waziri Rahma.

Aidha, Waziri huyo amesema kuwa katika kisiwa cha Pemba wananchi wake bado wana changamoto ya mawasiliano, hivyo wanapaswa kutatuliwa kero zao.

"Kisiwa kile kwa upande wa mawasiliano bado hakijawa vizuri kwa hiyo ninyi UCSAF kwa vile ni mfuko wa mawasiliano fanyeni jambo kwa maana awali nilikuwa sijauelewa mfuko huu ila kwa leo nimeweza kuufahamu,"amesema Rahma.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba ameelezea hatua wanazoendelea kuzichukua ili kuhakikisha huduma ya mawasiliano zinawafikia wananchi wote wa Zanzibar.

"Mfuko unaendelea kupambana ili kuweza kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana kote,na lengo ni kila sehemu kuwe na mawasiliano,"amesema Mashiba.

Hata hivyo, pamoja na Waziri huyo kutembelea mfuko huo pia amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya mfuko huo wa UCSAF linalojengwa katika eneo la Njedengwa jijini hapa.

Post a Comment

0 Comments