Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly awapa maarifa wanafunzi

Na Fresha Kinasa, Diramakini Blog

MJUMBE wa Baraza Kuu la Wanawake Tanzania (UWT) Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amewataka wanafunzi wa kike katika shule za sekondari mkoani Mara kujitambua na kusoma kwa bidii wanapokuwa shuleni badala ya kujiingiza katika vitendo vya anasa vitakavyowafanya wakatishe masomo na wasitimize ndoto zao kwa siku za usoni.
Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly akikabidhi taulo za kike kwa mmoja wa wanafunzi wa Sekondari Nyamunga iliyopo wilayani Rorya.
Rhobi ameyasema hayo kwa nyakati tofauti Oktoba 5, 2021 wakati akizungumza na wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Bukama na Nyamunga zilizopo Wilaya ya Rorya mkoani humo akiwa ameambatana na Wajumbe wa UWT wa wilaya hiyo katika kuadhimisha Siku ya UWT Taifa ambapo pia wameweza kugawa taulo za kike 242 zenye thamani ya Shilingi Milioni moja kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu.

Amesema, wanawajibu wa kujitambua na kutumia muda kipindi hiki wanasoma kwa usahihi kusudi waweze kufikia malengo. Huku akiwasisitiza wasikubali kurubuniwa na wanaume wakajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na hatimaye kupata madhara makubwa ya kiafya ikiwemo magonjwa ya kuambukiza pamoja na mimba na hivyo kutofikia ndoto zao kimaisha.

"Niwatake Wanafunzi wa kike kujitambua na kusoma kwa malengo, acheni tamaa kwa kutaka vitu vidogo vidogo kutoka kwa wanaume, ninyi ni wa thamani sana. Tumieni muda huu vyema mkiwa shuleni kusoma kwa bidii kusudi kwa baadaye mtoe mchango wa maendeleo kwa jamii na taifa letu. Tambueni kwamba mkijiingiza katika mahusiano kuna hatari ya kupata UKIMWI na mimba na hivyo hamtaweza kutimiza ndoto zenu,"amesema Rhobi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Rorya, Helen Pili Murya amesema jamii ina jukumu la kuhakikisha inashiriki vyema kuondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi wa kike. Huku akiwahimiza kutambua kwamba elimu ndio dira ya maisha yao, hivyo wasifanyiwe uzembe wa masomo.

Pia, amewataka kutambua kuwa, Wazazi wanatumia fedha kuwahudumia katika kuhakikisha kwamba wanafikia malengo yao. Hivyo jukumu lao ni kutumia vyema nafasi hiyo kusoma kwa bidii waje kuleta Mapinduzi chanya katika nyanja mbalimbali katika jamii kwa siku za usoni.

Naye Afisa Elimu Taaluma Idara ya Elimu Sekondari Wilaya ya Rorya, Joyce Tongori amewataka wanafunzi wa kike kujiepusha na matumizi ya simu za mkononi kwani muda wao haujafika. Akawaasa kutofuata mkumbo wa maisha na kujiepusha na marafiki wabaya ambao ni hatari kwa taaluma.
Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly akigawa taulo za kike.
Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly akizungumza,katikati kushoto kwake ni Mwenyekiti wa UWT Rorya, Helen Pili Murya
Ester Mponda ni Mwalimu mlezi wa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Bukama ameshukuru kwa msaada wa taulo za kike uliotolewa kwa wanafunzi shuleni hapo, ambapo amesema taulo hizo zitaimarisha mahudhurio ya watoto darasani kwani baadhi yao wanapokuwa hedhi hushindwa kuhudhuria shuleni hadi hedhi inapokoma na hivyo kupitwa na masomo.

Naomi Charles ni Mwanafunzi wa Kidato cha tatu shuleni hapo, ambapo amesema wanafunzi wa kike baadhi yao hutumia vitambaa kujisafisha wanapokuwa hedhi huku wengine wakishinda kukaa darasani kwa muda wote kutokana na kukosa taulo za kujistili ameomba wadau mbalimbali kusaidia kutatua changamoto hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa kike katika Sekondari ya Bukama iliyopo Rorya wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa UWT Wilaya ya Rorya pamoja na Mjumbe wa UWT Taifa Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kinesi Kata ya Nyamuga na kuhudhuriwa na wajumne wa UWT pamoja na Wananchi wa kata hiyo, Rhobi amewaomba Wanawake kuunda vikundi na kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo hutolewa Halmashauri ili kujikwamua kiuchumu. Huku akisisitiza pia kupinga vitendo vya kikatili kuanzia ngazi ya familia katika Kujenga usawa na ushirikiano.

Aidha, amewahimiza wanachama wa CCM kujiandikisha kwa mfumo wa TEHAMA na kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan sambamba kuyasema yale yote yanayotekelezwa na chama cha Mapinduzi kwa manufaa ya watanzania.

Post a Comment

0 Comments