Mkinga yaendelea kutafuta ufumbuzi uhaba wa vyumba vya madarasa

Na Hadija Bagasha, Mkinga

HALMASHAURI ya wilaya ya Mkinga inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 442 kwa shule za msingi huku kwa upande wa sekondari ikiwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 13 vinavyohitaji kujengwa ambavyo vitasaidia kuwezesha wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani.
Uwepo wa vyumba hivyo vya madarasa vya kutosha unatarajiwa kuwasaidia watoto wa kike kuepukana na mimba za utotoni lakini pia kujikita vizuri katika masomo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa hamalshauri hiyo, Zahara Msangi ameelezea uhaba uliopo kwa upande wa shule za msingi huku kwa upande wa sekondari ni vyumba 13 vinavyohitajika.

Mkurugenzi Zahara amesema, wilaya hiyo suala la elimu wanalipa kipaumbele kwani lengo la Halmashauri zao ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora lakini pia huduma zinawafikia kwa karibu zaidi.

"Katika suala la elimu kitu kikubwa kinachowezesha wananfunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia ni madarasa tunayo changamoto kubwa ya madarasa kwa sekondari na msingi lakini pia tuna changamoto ya madawati ila tunawashukuru wenzetu wa World Vision kwa kutupatia msaada wa madawati 150 na tumeshayasambaza katika shule mbalimbali za msingi wilayani kwetu, "alisema Mkurugenzi Msangi.

Alisema, mahitaji ya madarasa waliyo nayo kwa shule za msingi ni 771 huku yaliyopo hivi sasa ni 499 kitendo ambacho kinaonyesha bado wana uhitaji mkubwa ambao ni kama madarasa 442.

"Wenzetu wa World Vision wameweza kusaidia kupunguza hiyo changamoto kwa kiwango fulani hivyo nitumie nafasi hii kuwaasa wadau wengine kutusaidia kupata madarasa haya zaidi ya 400 tunayohitaji, laini pia nitumie nafasi hii kumshukuru mheshimiwa Rais Samia kwa kutuwezesha kupata fedha zitakatusaidia kuongeza, madarasa katika shule za msingi na sekondari, "amebainisha.

Katika kukabiliana na changamoto hii jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ambapo Kaimu Afisa elimu Sekondari wilayani humo Rose Godwin amesema kutokana na changamoto hiyo halmashauri imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha upungufu huo unapungua.

Alisema, Halmashauri hiyo kupitia mapato ya ndani imekuwa ikitenga bajeti ambayo inapeleka kipaumbele katika shule husika yenye mahitaji makubwa ya madarasa.

"World Vision wamekuwa wadau muhimu sana kwetu katika kutusaidia changamoto hii kwani wamejenga sehemu zilizokuwa na changamoto kubwa kwa mfano Kibiboni, Mtimbwani hii imesaidia kupunguza msongamano madarasani lakini pia kutembea umbali mrefu, "alisisitiza Rose.

Katika kukabiliana na uhaba huo shirika la maendeleo la World vision Tanzania wanasema katika miradi hii wametumia milioni 180 kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

Awali akizungumza na kituo hiki meneja mradi world vision Mkinga Evodia Chija amesema baada ya kujenga madarasa hayo matarajio yao ni ufaulu kuongezeka.

Alisema katika kushirikiana na serikali wamefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani baada ya kutengeneza mradi mkubwa wa maji wa milioni 271 eneo la Duga wilayani humo huku eneo la Doda na Kibiboni wakiwa na mradi wa milioni 400.

Evodia alisema miradi yote hiyo inakwenda kusaidia watoto zaidi ya 1000 ambao walikuwa hawaendi shule kwa wakati kwa ukosefu wa maji lakini pia utasaida wazazi kufanya shughuli za kujiingizia kipato kutokana na muda mwingi walikuwa wakiutumia kutafuta maji.

Ni ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na shirika la World vision katika wilaya ya Mkinga uku miradi inayotembelewa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu katika shule za msingi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news