Mtaalam: Mwaka 2030 tatizo la afya ya akili duniani litaongezeka kwa asilimia 17

Na Doreen Aloyce, Dodoma

IMEBAINISHWA kuwa mpaka kufikia mwaka 2030 tatizo la afya ya akili duniani litaongezeka hadi kufikia asilimia 17 kutoka asilimia 12 na endapo jamii ikasimamia suala la malezi na makuzi tatizo hilo litapungua hadi kufikia asilimia moja.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani na kupinga matumizi ya pombe kupita kiasi Oktoba 10, mwaka huu, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya anayeshughulikia Magonjwa yasiyoambukiza Dkt. James Kihologwe amesema, suala la afya ni mtambuka katika malezi na kila mmoja anao wajibu wa kufanya tatizo hilo lipungue.

Aidha, Kihologwe ameeleza kuwa suala la tatizo la afya ya akili huchangiwa na sababu nyingi ikiwemo na unywaji wa pombe uliopitiliza utumiaji wa madawa ya kulevya,mawazo, sonona na sababu nyingine nyingi.

"Athari ya pombe na madhara yake ni makubwa ambapo takwimu zinaonesha tuna tatizo kubwa la vifo milioni 3 vinavyotokana na pombe duniani huku wengine wakiwa na ulemavu wa maisha,"amesema Dkt.Kihologwe.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Shedrack Makubi amesema, takwimu zinaonesha Tanzania kuna wagonjwa wa afya ya akili milioni saba.

"Tunatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuwekeza zaidi katika magonjwa ya akili, afya ya akili kwani tatizo hili limeonekana kukuwa siku hadi siku,"amesema Dkt.Makubi.

Paul Lawala ni Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Afya ya akili Mirembe amebainisha kuwa, licha ya jitihada zinazofanyika bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa wataalamu wa afya za akili.

Pia amebainisha changamoto ya miundombinu ambayo iliyopo kwa sasa haikidhi mahitaji ya huduma zinazotolewa kwani imechakaa hasa barabara zinazoingia sehemu za kutolea huduma.

Ametoa wito kwa jamii kuacha kuwanyanyapaa wagonjwa wa afya ya akili, kwani ni wagonjwa kama wagonjwa wengine na wanastahili haki anazostahili mgonjwa yoyote na muwasihi kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma mara waonapo dalili za ugonjwa.

"Tunaomba Serikali itusaidie kuwasomesha wataalamu wa afya za akili katika fani hiyo na kuwaajiri huku wakipewa mazingira mazuri ya kazi jambo ambalo litasaidia kurahisisha kazi,"amesema.

Nae Mbunge wa Shinyanga kupitia Viti Maalumu,Salome Makamba ameitaka jamii kuamimi kwamba ugonjwa wa akili unatibika na kuacha imani potofu za kuwapeleka wagonjwa kutibiwa kwa waganga wa kienyeji na badala yake wagonjwa wote wenye changamoto hiyo wapelekwe katika Hospitali ya Mirembe iliyopo Dodoma.

"Kwenye jamii yetu bado tuna changamoto kubwa,ukweli usiopingika elimu juu ya magonjwa ya afya ya akili ni mdogo na wengi hudhani kwamba ukipata tatizo la akili huwezi kupona jambo ambalo sio la kweli,

"Sasa hivi Serikali ipo kwenye mchakato kupitisha muswada ili iwe sheria ya bima ya afya kwa kila mtanzania lazima awe na bima ya afya na mimi kama mbunge mwakilishi wa wananchi napendekeza ugonjwa wa akili uingie kwenye matibabu ya bima ya afya,"amesema Salome.

Post a Comment

0 Comments