Muheza wataja sababu ya kuuza chungwa moja kwa 10/- mbele ya DC Halima Bulembo

Na Hadija Bagasha, Muheza

Changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika kijiji cha Mto wa Mbuzi Kata ya Mhamba wilayani Muheza imechangia wafanyabiashara wa machungwa kuuza chungwa moja kwa shilingi 10 kitendo ambacho kimekuwa kikiwaletea hasara wakulima wa zao hilo.
Kufuatia hatua hiyo, wakulima hao wa machungwa wameiomba serikali kuwaharakishia ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa kilimo hicho ndio wanachokitegemea kuendeshea maisha yao.

Wakulima hao wametoa kilio hicho wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo alipofika kijijini huko kama sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kata kwa kata, kijiji kwa kijiji kwa lengo la kujitambulisha kwa wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya wakulima wengine wa machungwa, walisema kuwa wilaya hiyo machungwa ndio zao pekee linalotegemewa na wananchi kuwaingizia kipato hivyo ifike wakati sasa serikali ione kuwa wanafanya kilimo chao kwa hasara.

"Mheshimiwa mkuu wetu wa wilaya tukuombe utufikishie salamu zetu serikalini kwa kuwa wakulima wa machungwa Muheza tunapata hasara kubwa sana kitendo cha kuuza chungwa moja shilingi 10 ni hasara kubwa sana, lakini hatuna namna barabara zetu ndio zinazopelekea sisi tupate hasara,"walisema wakulima hao.

Waliongeza kuwa, machungwa yao ya Muheza yanategemewa katika mikoa mbalimbali hapa nchini, "lakini cha ajabu wakulima sisi tumekuwa hatufaidiki na kilimo chetu, hivyo serikali ituangalie wananchi wake tunatumia nguvu nyingi mashambani, lakini faida hakuna,"walisema.

Katika hatua nyingine wananchi hao wamempongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa kuweza kufika kijijini humo na kujionea changamoto wanazokabiliana nazo wananchi hao huku wakiahidi kumpa ushirikiano wa kutosha na kusema kuwa maendeleo hayaji bila kushirikiana kati ya viongozi waliopo na wananchi wake hivyo wapo tayari kumpa ushirikiano.

Awali akizungumza mara baada ya kutembelea kijiji hicho na kusikiliza kero za wananchi Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Bulembo amekiri kweli kuwepo kwa changamoto hiyo ya barabara ambapo amewaomba wananchi wawe na subira wakati serikali ikiendelea na mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

"Ndugu zangu wananchi niwaombe tu muwe wavumilivu kwa serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwakwamua wananchi wake na umaskini, hivyo ni serikali sikivu ambapo hivi sasa tunashuhudia namna ambavyo serikali imekuwa ikitoa fedha kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu na afya,"amesisitiza DC Bulembo.

Bulembo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hasan kwa kuipatia wilaya hiyo sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa, pamoja na sekta ya afya.

Hata hivyo, DC Bulembo alisema kuwa ni wakati wa wazazi sasa kuwasimamia watoto wao maendeleo ya shule kwani serikali kila kukicha imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto zilizopo katika sekta hiyo ya elimu.

Bulembo amesema kuwa, hatomvumilia mzazi yeyote atakayediriki kumkatisha mtoto wake shule iwe wa kike au wa kiume kwa ajili ya kumuozesha au kumfanyisha biashara yeyote mitaani kwa ajili ya kuwaingizia kipato kitendo ambacho kimekuwa kikikatisha ndoto za wanafunzi wengi.

Sambamba na hayo, DC Bulembo amekemea vikali baadhi ya wananchi kijijini hapo kujihusisha na uuzaji na matumizi ya biashara ya bangi ambapo ameahidi kuwachukulia hatua kali za sheria wale wote watakaotajwa kujihusisha na biashara hiyo pindi atakapojiridhisha.

Mbali na hayo mkuu huyo wa wilaya alisema mgawo wa ujenzi vyumba vya madarasa shule za sekondari wilayani Muheza mahitaji 96, vilivyopo 39, upungufu 57, idadi ya vyumba walivyopewa ni 57 ambapo kila darasa limepewa milioni 20 jumla kuu ni bilioni 1.140.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mchanganuo wa miundombinu ya vyumba vya madarasa itakayojengwa kwenye shule shikizi ni vituo vitatu, idadi ya vyumba vya madarasa katika shule shikizi ni 10 ambapo kila darasa moja limepewa milioni 20 na kufikia jumla ya milioni 200.

Alisema,orodha ya shule za msingi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu zinazopendekezwa kujengewa miundombinu, idadi ya mabweni ni 1 na kiasi walichopewa ni milioni 80 na jumla kuu ni milioni 80.

Aidha alisema kuwa Muheza ni moja ya Halmashauri itakayopata chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ambapo watapatiwa milioni 100 kwajili ya ujenzi wa chumba hicho.

Jumla kuu ya idadi ya fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali wilayani humo ni bilioni 1.520.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news