Mwanafunzi darasa la saba aipatia shule Milioni 4/-

Na Robert Kalokola,Geita

Mwanafunzi wa Darasa la Saba Shule ya Msingi Nguzombili Halmashauri ya Mji wa Geita,  Viktoria Michael amechaguliwa kuwa mchoraji bora wa mchoro wa alama za usalama barabarani katika mafunzo ya usalama barabarani mkoani Geita na kusababisha shule yake kupewa milioni nne za mradi wa maendeleo na yeye mwenyewe kupata laki tano.
Wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Nguzombili wakionyesha kombe baada ya Mwanafunzi Viktoria Michael kushinda uchoraji bora wa alama za usalama barabarani. (Picha na Robert Kalokola).
Masumbuko Stephano kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Geita ( wa tatu kutoka kushoto) na Afisa Usalama na Mazingira wa Puma Energy (mwenye koti jeusi) wakiongoza timu ya kuchagua mshindi wa mchoro wa alama za usalama barabarani. (Picha na Robert Kalokola).

Mwanafunzi huyo ametangazwa na Ambokege Minga ambaye ni Afisa Usalama na Mazingira wa Kampuni ya Puma Energy Oktoba 20,mwaka huu katika Uwanja wa shule ya Msingi Kalangalala mjini Geita wakati wa kutangaza wanafunzi kumi bora walioshiriki mafunzo ya usalama barabarani mkoani Geita yaliyoendeshwa na shirika la Amend kwa ufadhili wa Puma Energy.

Shirika hilo limeendesha mafunzo hayo katika mikoa mitano ambayo ni Dar es Salaam,Geita,Ruvuma ,Dodoma Kilimanjaro na Visiwa vya Zanzibar ambapo wanafunzi 110,000 kutoka katika shule za msingi zaidi ya 100 wamepata mafunzo ya elimu ya usalama barabarani ,lengo likiwa kupunguza ajali za barabarani nchini kwa wanafunzi na janii kwa ujumla.
Mwakilishi wa Afisa elimu mkoa wa Geita Masumbuko Stephano akikabidhi zawadi ya laki 5 kwa mwanafunzi aliyemwakilisha Viktoria Michael. (Picha na Robert Kalokola).

Mshindi wa kwanza wa mashindano hayo ya kuchora mchoro wa usalama barabarani Victoria Michael licha ya kuipatia shule yake milioni 4 pia ametunukiwa laki tano na mshindi wa pili zabibu Stanford Shule ya msingi Nyankumbu aliyepata Sh.300,000 na mshindi wa tatu ni Paul Haruna wa shule ya Msingi Nguzombili aliyepata Sh.150,000.

Wanafunzi wengine saba kila mmoja amepata zawadi ya elfu thelathini na begi la shule pamoja na madaftari ambao niMathias Daniniel (shule ya msingi Nyankumbu),Dorcus Kasazo (Lukaranga), Deus Deus (Kalangalala),Justine Mabula(Mwatulole), Grace Mabula(Lukaranga) na Majura Bahati (Nguzombili).

Kampuni ya Puma amesema, wameamua kuja Geita kwa sababu ya ukuaji wa haraka wa mji huo ambapo shughuli za kijamii na ongezeko la watu na magari ambayo yanahatarisha usalama wa watoto wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.
Masumbuko Stephano kwa niaba ya Afisa elimu mkoa wa Geita akikabidhi kombe kwa mwalimu wa Shule ya msingi Nguzombili. (Picha na Robert Kalokola).

Akifafanua zaidi Ambokege Minga amesema, Puma Energy Tanzania Ltd imetoa zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi walioshinda shindano la michororo ya usalama barabarani kwa mwaka 2020-2021 mkoani Geita na kwamba tukio hilo la utoaji zawadi linahitismisha mradi huo kwa kipindi cha mwaka huu uliofanywa Kampuni ya Puma kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la Amend.

"Mpango huu katika Mkoa wa Geita ulihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani katika shule tano na wanafunzi wasiopungua 12,000 wamefikiwa pamoja na shindano la uchoraji wa michoro inayo hamasisha usalama barabarani.

Afisa Elimu Mkoa wa Geita kupitia kwa mwakilishi wake Masumbuko Stephano amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu hivyo ni vizuri Puma wakaendelea kutoa kwani elimu hiyo ni muhimu yenye lengo la kuokoa maisha ya watu.

"Tunapotoa mafunzo kwa wanafunzi maana yake tunakwenda kupeleka elimu hiyo ngazi ya chini kabisa, wanafunzi ambao tunawaona shuleni wana wazazi na walezi wao ndio sisi,"amesema.
Picha ya pamoja baada ya kukabidhi kombe na zawadi kwa wanafunzi Bora katika uchoraji wa alama za barabarani. (Picha na Robert Kalokola).

Pia amesema wamefurahishwa na shindano la michoro kutoa elimu ya usalama barabarani na kubwa zaidi zawadi ya Sh.milioni nne ambayo shule itakayotoa mshindi wa kwanza itatoa hamasa kwa shule kuwa mabalozi wazuri, lakini kwa mwanafunzi atakayeshinda na kushika nafasi ya kwanza kwa uchoraji.

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Nguzo Mbili amesema siri ya ushindi wa shindano hilo ni kujamini ,kujituma na kuwapa wanafunzi kutambua namna ya kutumia vipaji vyao na hatimaye wameibuka kidedea na kushinda Sh.Milioni Nne wakati mshindi wa kwanza kutoka shule hiyo ameibuka mshindi kwa kuchukua nafasi ya kwanza na kushinda 500,000.

Kwa upande wake Mkaguzi Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Geita Emmanuel Shagaya amewaomba wanafunzi waliopata mafunzo hayo kufikisha ujumbe unaohusu usalama barabarani kwa kufundisha wenzao lakini na kuwaeleza wazazi wao kuhusu usalama barabarani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news