OFISI YA MSAJILI WA JUMUIYA, WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI IMEWATAKA VIONGOZI WA VYAMA, TAASISI NA VIKUNDI KUHUISHA USAJILI WA VYAMA VYAO KABLA YA NOVEMBA 30 MWAKA HUU

NA MWANDISHI MAALUM

Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imewataka viongozi na wanachama wa vyama, vikundi na taasisi zote zisizo za kidini zilizopo Mikoa ya Kanda ya Ziwa kufika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kuhuisha vyeti vyao vya usajili kabla ya Novemba 30,2021.
Aidha, imesema zipo jumuiya nyingine ambazo usajili wao utafutwa kwa mujibu wa sheria endapo hawatoshiriki katika zoezi hilo huku ikivitaka vyama na vikundi vyote vyenye sifa ya kusajiliwa kufika ili wapewe utaratibu wa kusajiliwa.

Agizo hilo limetolewa na Emmanuel Kihampa ambaye ni Msajili Wa Jumuiya, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Oktoba 22, 2021 Jijini Mwanza wakati akizungumza ndani ya kipindi cha Morning Express kinachorushwa na Kituo cha Radio City fm 90.5 Mwanza kuhusu zoezi la kuhuisha vyeti vya Jumuiya zisizo za kidini kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema,  ofisi yake ilianza kazi tangu mwaka 1955 na ndiyo wenye dhamana ya kusajili Makanisa, Misikiti na taasisi na mashirika ya kidini, vyama na vikundi vyote vya kijamii na hivyo wameamua kusogeza huduma zao kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kupunguza safari ya kufata huduma hiyo Mkoani Dodoma.

Akitolea mfano wa jumuiya zisizo za Kidini Kihampa amezitaja kwenye makundi manne ambayo ni Jumuiya za Kitamaduni akitolea mfano vyama vya kikabila, Jumuiya za kiuchumi ambazo zinajihusisha na shuhuli za kiuchumi mfano bodaboda, wajasiriamali, Jumuiya za Kijamii vyama vya kusaidiana mfano vya kufa na kuzikana na Jumuiya za Kitaaluma ambazo ni zile za wanataaluma mfano mafundi simu nk.

Akizungumzia lengo la zoezi hilo linaloendelea mkoani Mwanza amesema ni kubaini uhai wa Jumuiya kwani tangu mwaka 1955 mpaka kufikia mwezi Julai 2021 orodha ya Jumuiya zilizopo ni 9,868 lakini wakija kuangalia kwenye utekelezaji wa usaji wamebaini zaidi ya asilimia 50 ya Jumuiya hazionekani.

“Lengo la pili ni kutaka kufahamu hizi Jumuiya ambazo zipo zinajiendeshaje tutataka kuangalia katiba wanazotumia , malengo yao na taratibu za uendeshaji je unawapa sifa za kuendelea kubaki kwenye regista ya usajili Wizara ya Mambo ya ndani au tayari wameshapotweza sifa na je malengo na taratibu za uendeshaji yanaenda sambamba na sheria za Jumuiya na sharia nyingine za nchi yetu.

“Malengo mengine ni kutaka kubaini kama hizi Jumuiya zinazingatia kikamilifu masharti ya Usajili ambayo yanahusisha uandaaji wa nyaraka, ulipaji wa tozo mbalimbali pamoja na mabadiliko ya uongozi sambamba na maelekezo ya Katiba zao,”ameongeza.

Amesema, zoezi la kuhuisha usajili wa vyama, vikundi na taasisi kwa hapa Mwanza limeanza Oktoba 20, 2021 na litafika tamati Oktoba 28, 2021 na kwa wale wanaotaka kuhuisha wanatakiwa kufika na nyaraka zikiwemo cheti cha usajili, taarifa za fedha, taarifa ya mabadiliko ya uongozi, uthibitisho wa malipo ya ada pia watataka kuona katiba na kanuni ambazo wanazitumia katika uendeshaji wa shughuli zao.

Amesema wale wote ambao hawatojitokeza kushiriki zoezi hilo hadi kufikia Novemba 30 mwaka huu vyeti vyao vitakuwa batili na watashindwa kuvitumia na wale wote ambao watahitaji maelezo na ufafanuzi Zaidi wanaweza kupiga simu namba 0734 712744 au barua pepe rs@moha.go.tz

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news