Rais Dkt.Mwinyi ateta na Balozi wa Comoro, Namibia na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Muuungano wa Visiwa vya Comoro hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya biashara.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Dkt.Ahamada El Badoi Mohamed Fakih.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahamada El Badoi Mohamed Fakih wakati wa mazungumzo yao alipofika Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Balozi Fakih kwamba kutokana kuwepo kwa mahusiano ya kidugu baina ya pande mbili hizo ni kichocheo pekee cha wafanyabiashara wa Zanzibar na Comoro kuimarisha sekta ya biashara hasa kutokana na muingiliano wa kidugu uliopo.

Hivyo, Rais Dkt.Mwinyi alimuhakikishia Balozi Fakih kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake itaendeleza na kudumisha uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo sambamba na kuendeleza sekta za uchumi kwa mashirikiano ya pamoja kwa maslahi ya nchi mbili hizo na watu wake.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akibadilishana mawazo na Mgeni wake Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahamada El Badoi Mohamed Fakih baada ya mazungumzo yao aliyofanyika leo Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Naye Balozi wa Muungano wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Dkt. Ahamada El Badoi Mohamed Fakih alimueleza alimueleza Rais Dkt.Mwinyi haja ya kurudisha utamaduni wa wafanyabiashara wa Comoro kuja kufanya biashara Zanzibar na wale wa Zanzibar kwenda nchini Comoro kwa ajili ya kufanya biashara.

Balozi Fakih alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dkt.Mwinyi uhusiano na ushirikaiano wa kihistoria uliopo kati ya Comoro na Zanzibar ambao una kila sababu ya kuimarishwa zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Aidha, Balozi Fakih alimueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya nchi yake ya kutekeleza Mkataba wa Makubaliano yaliyokubaliwa kati ya Zanzibar na Comoro katika uongozi wa awamu iliyopita huku akitoa shukurani kwa huduma kadhaa wanazozipata wananchi wa Comoro katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo huduma za afya, elimu na nyinginezo.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Namibia Nchini Tanzania Mhe.Lebbius Tangeni Tobias alipofika Ikulu jijini Zanzibar.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Lebbius Tangeni aliyefika Ikulu kujitambulisha ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walisisitiza haja ya kuwepo mashirikiano ya pamoja hasa katika uendelezaji wa sekta za kiuchumi ikiwemo viwanda, biashara, uwekezaji pamoja na mahusiano ya Miji na Manispaa za Zanzibar na Namibia.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Tangeni alimueleza Rais Dkt. Mwinyi hatua na juhudi za makusudi alizoanza kuzichukua za kuazimia kukutana na uongozi wa ngazi za mikoa wa Zanzibar pamoja na viongozi wa Manispaa na Jiji la Zanzibar kwa azma ya kuweka mahusiano na ushirikiano kati yao na ndugu zao wa Namibia katika maeneo hayo.

Balozi Tangeni alieleza kwamba mbali ya azma yake hiyo ya kukutana na viongozi hao pia, ana lengo la kukutana na uongozi wa Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), ili kuweza kushirikiana na kuleta mahusiano pamoja kati ya Mamlaka hiyo na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Namibia.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akibadilishana mawazo na mgeni wake Balozi wa Namibia nchini Tanzania, Mhe.Lebbius Tangeni Tobias baada ya mazungumzo yao aliyofanyika leo Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Aidha, Balozi Tangeni alieleza mashirikiano ya kihistoria yaliopo kati ya Namibia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yameasisiwa na viongozi wakuu wa nchi mbili hizo tokea wakati wa kudai uhuru ambayo yanahitaji kuimarishwa zaidi.

Naye Rais Dkt. Mwinyi kwa upande wake alimueleza Balozi huyo wa Namibia, Dira ya Serikali anayoiongoza ya Uchumi wa Buluu na kusisitiza kwamba Namibia ina nafasi nzuri katika kushirikiana na Zanzibar kwenye dira hiyo hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vya samaki.

Mapema, Rais Dkt.Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Dk. Elieza Mbuki Feliesh ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha, alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi huku akieleza azma yake ya kuimarisha kada ya sheria hasa kwa vijana hapa nchini.

Rais Dkt.Mwinyi kwa upande wake alimpongeza Jaji Felesh kwa kupata uteuzi huo na kueleza imani yake kwamba kiongozi huyo atafanya kazi kwa ustadi kubwa kutokana na uzoefu alionao huku akieleza muingiliano uliopo kwenye sekta ya sheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unahitajia mashirikiano ya pamoja kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news