Rais Dkt.Mwinyi awaeleza ukweli viongozi wa Serikali za mitaa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa yakiwemo Mabaraza ya Miji na Manispaa za Zanzibar.
Rais ameyasema hayo alipokutana na viongozi wa Serikali za Mitaa kutoka mikoa yote ya Zanzibar wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote za Unguja na Pemba, Ikulu jijini Zanzibar.

Ameeleza kwamba, lengo la kikao hicho ni kuhakikisha mabadiliko chanya yanatokea hasa katika Halmashauri za Unguja na Pemba sambamba na kuimarisha utendaji wa kazi kwa azma ya kuwahudumia ipasavyo wananchi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza haja kwa kila Halmashauri ihakikishe inatekeleza ipasavyo majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuzisimamia fedha za makusanyo ya mapato na kuwataka Wakuu wa Mika na Wilaya kusimamia hilo ili fedha hizo ziweze kusaidia shughuli za maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi aliyaeleza majukumu ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kusimamia suala zima la usafi katika maeneo yote ya Miji ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni eneo maarufu la utalii.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba makusanyo ya Halmashauri ni lazima yatumike kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza jukumu la Manispaa zote za Unguja na Pemba katika kuhakikisha miji inakuwa safi huku akiutaka uongozi wa Tamisemi kuwashajiisha wananchi kufanya usafi katika maeneo yote wanayoishi yakiwemo maeneo ya biashara.

Alieleza haja kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kupangwa vizuri na kusisitiza kufanya biashara katika maeneo maalum yaliyopangwa.

Rais Dkt. Mwinyi pia, alieleza azma yake ya kuendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono Wajasariamali kwa kutoa kiasi cha fedha zipatazo Bilioni 70 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kuwasaidia ambapo wenye jukumu la kusimamia fedha hizo ni Serikali za Mitaa.

Pamoja na hayo, Rais Dkt. Miwnyi alieleza jukumu la Uongozi wa Mikoa na Wilaya la kusimamia suala zima la ulinzi na usalama ili kuhakikisha vitendo viovu vinakomeshwa katika jamii.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza haja kwa Masheha wa Shehia zote za Unguja na Pemba kutekeleza shughuli zao kwa uadilifu zaidi ili kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo katika maeneo yao.

Nao viongozi hao wa Serikali za Mitaa walitoa pongezi zao kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa maelekezo mazuri aliyowapa pamoja na kuwatia moyo katika utendaji wao wa kazi na kuahidi kuleta mabadiliko katika kipindi kifupi kijacho.

Post a Comment

0 Comments