RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI KILELE CHA WIKI YA UWT WILAYANI RUFIJI

Na Rotary Haule,Pwani

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya wiki ya Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) yatakayofanyika Oktoba 23, mwaka huu Rufiji mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa UWT, Gaudensia Kabaka amewaambia waandishi wa habari leo Mjini Kibaha kuwa maandalizi juu ya sherehe hizo yamekamilika na wamejipanga vizuri katika kuadhimisha siku hiyo.

Kabaka,amesema kuwa kwa kawaida maadhimisho ya wiki ya UWT hufanyika kila mwaka kuanzia Septemba 27 mpaka Oktoba 4 lakini walilazimika kusogeza mbele kutokana na ratiba za mgeni rasmi kubana na hivyo kupata nafasi Oktoba 23.

Amesema,katika kuadhimisha kilele hicho kwa sasa UWT inaendelea na kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Rufiji kwa kutoa misaada katika Shule mbalimbali ikiwemo Ikwiriri Sekondari na kutembelea vituo vya afya kwa kutoa shuka na vifaa vingine.

Amesema,wameamua maadhimisho hayo yafanyike wilayani Rufiji kutokana na kutaka kumuenzi na kukumbuka juhudi za mwanamke shupavu mpigania Uhuru Bibi Titi Mohamed ambaye wazazi wake walizaliwa Rufiji.

"Bibi Titi Mohamed alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa UWT na mwanamke wa kwanza shupavu aliyefanya mapambano ya kupigania Uhuru wa nchi yetu kwa hiyo sisi UWT tumeona tumuenzi kupitia maadhimisho haya,"amesema Kabaka.

Aidha,Kabaka amesema kuwa wanapomuenzi Bibi Titi, lakini pia wanakumbuka na kupongeza juhudi za Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ni Rais mwanamke anayefanya mambo makubwa ambayo yanaifanya nchi ya Tanzania kung'ara kimataifa.

Amesema kuwa,Rais Samia ambaye ameonyesha namna ambavyo anaweza kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo inakamilika pamoja na kuweka juhudi kubwa katika suala la Uviko-19.

"Rais Samia ni mama shupavu ambaye ametoa Trilioni 1:3 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendana na mambo ya Uviko 19 ikiwemo hospitali,Shule na miundombinu ya barabara kwahiyo tunapoazimisha pia tunamsapoti Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya,"amesema Kabaka
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amesema kuwa ameishukuru UWT kwa kufanya maamuzi ya kufanyia maadhimisho hayo Mkoani kwake na kwamba itakuwa historia kubwa Mkoani Pwani.

Kunenge,amesema kuwa sherehe hizo zitasaidia kuufungua Mkoa wa Pwani hasa katika kujifunza historia iliyopo kutokana na umaarufu na ushupavu wa Bibi Titi Mohamed na hivyo kuwa sehemu ya kukuza utalii Mkoa wa Pwani

Amesema,Mkoa wa Pwani unaungana na UWT kwa maadhimisho hayo lakini pia wanaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwakuwa ni Rais Shupavu na anafanyakazi kubwa Mkoa wa Pwani na Taifa kiujumla.

Kunenge ,amesema kwa Mkoa wa Pwani tayari mpaka sasa wamepokea fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hata katika kukabiliana na janga la Uviko-19 huku akitaja miradi mingine mikubwa ya kimkakati.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa bandari kavu ya Kwala,mradi wa bwawa la kufua umeme huko Rufiji,daraja la Wami pamoja na miradi mingine mikubwa ya kimaendeleo.

Nae Katibu Mkuu wa UWT Philis Nyimbi, amesema Jumuiya inaendelea kuweka misingi imara kuanzia ngazi ya chini kwa ajili ya kuhakikisha wanapata wanachama wengi zaidi.

Nyimbi,amesema tangu mwaka 2017 mpaka sasa Jumuiya imekuwa na zaidi ya wanachama milioni 2 ambapo mikakati iliyopo ni kuwaunganisha Wanawake kote nchini mpaka ngazi ya Vijijini.

Post a Comment

0 Comments