Serikali yaagiza wavamizi eneo la FARM CHAMWINO kuondoka ndani ya wiki mbili

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Serikali imeagiza wananchi waliovamia eneo la Farm katika Kijiji cha Chamwino Ikulu mkoani Dodoma kuondoka katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Oktoba 2, 2021 kwa kuwa kijiji hicho kilishatangazwa eneo la mpango mwaka 1992 kupitia GN Na 263 ya tarehe 25 Juni 1992 ili kuepusha sheria ya ardhi ya vijiji (Sura 114 Toleo la 2002) kutumika.
Mkuu wa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma Gift Msuya (aliyenyoosha kidole) akimuelekeza jambo Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino Enock Mligo (kulia) wakati akikagua eneo lililovamiwa na wananchi wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi katika eneo la Farm kijiji cha Chamwino Ikulu tarehe 1 Oktoba 2021.
Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge akifafanua jambo kwa Mkuu wa wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma Gift Msuya wakati wa kukagua eneo la Farm lililovamiwa na wananchi katika kijiji cha Chamwino Ikulu tarehe 1 Oktoba 2021.

Agizo hilo limetolewa leo Oktoba 1, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Gift Msuya wakati wa kutangaza maamuzi ya timu ya uchunguzi wa mgogoro wa eneo la Farm mbele ya wananchi wa kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma.

"Natoa tamko la serikali kwa niaba ya kamati ya ulinzi ya wilaya na wananchi wa kijiji cha Chamwino naagiza wanaokalia maeneo ndani ya eneo la Farm kuondoka ndani ya wiki mbili na watakaokaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao" alisema Gift Msuya.
Mkuu wa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma Gift Msuya akizungumza wakati wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi kwenye eneo la Farm kijiji cha Chamwino Ikulu Dodoma tarehe 1 Oktoba 2021. Wa pili kushoto ni Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge na kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge.

Sehemu ya eneo la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari 640 lililoanzishwa kati ya mwaka 1971/1972 na Hayati baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuwafunza wanakijiji cha Chamwino ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe na kuku lilivamiwa na kuzua mgogoro kati ya wananchi na serikali.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Chamwino, mwananchi yeyote aliyeingia ndani ya eneo hilo ni marufuku kufanya shughuli yoyote kama vile ujenzi, kilimo na serikali kupitia idara ya ardhi itaweka mabango katika eneo hilo kuonesha kuwa eneo hilo ni eneo la umma.

‘’Wanaoendelea kufanya ujenzi watakuwa wanajiingiza hasara na wananchi mwenye yeyote mwenye nyaraka za kumilikishwa sehemu ya eneo hilo la Farm afike ofisi ya mkuu wa wilaya na atapatiwa haki yake,"amesema Gift Msuya.
Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge akizungumza wakati wa kikao cha kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi katika eneo la Farm kijiji cha Chamwino Ikulu tarehe 1 Oktoba 2021.

Kwa upande wake Kamishna wa ardhi nchini Nathaniel Nhonge alisema, kumbukumbu katika eneo hilo zimeweka bayana kuwa, eneo lenye mgogoro la Farm lilitolewa kwa matumizi ya umma na hakuna mabadiliko yaliyofanyika kwenda kwa mtu mmoja mmoja.

"Kimsingi hakuna mtu aliyelipwa fidia ndani ya eneo la Farm na wale wananchi waliolipwa kimakosa wanatakiwa warejeshe fedha,"amesema Nhonge.

Alisema, baada ya ripoti ya tume ya uchunguzi kuhusiana na mgogoro huo sasa upimaji utafanyika eneo lililotolewa kwa matumizi ya taasisi za shule ya sekondari Chamwino, Shule ya Msingi Kikwete pamoja na eneo la Mahakama na kuyamilikisha kwa wahusika kuepuka migogoro hapo baadaye.

"Serikali itaweka utaratibu wa kudumu wa kubaini na kulinda maeneo mengine ya aina hii yaliyoko ndani ya Chamwino dhidi ya uvamizi wa wananchi". alisema Kamishna Nhonge.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Chamwino Ikulu mkoani Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Chamwino Gift Msuya (hayupo pichani) wakati wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi eneo la Farm kijiji cha Chamwino tarehe 1 Oktoba 2021

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chamwino wameonesha kutoridhishwa na maamuzu hayo kwa kueleza kuwa maeneo hayo walirithi na kuridhiwa na serikali ya kijiji kwa nyakati tofauti ingawa hawakuwa na nyaraka zozote zinazoonesha kumilikishwa maeneo hayo.

Eneo la Farm katika kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma limekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu uliosababisha kuundwa kwa timu maalum ya kushughulikia mgogoro huo.

Wakati wa kushughulikia mgogoro timu ya uchunguzi ilielezwa kuwa, shamba la Farm lilitolewa kwa serikali ya kijiji miaka ya 1971/1972 kwa matumizi ya mradi wa mifugo na baada ya mradi kufa mwaka 1995 baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo kabla ya Farm kuanzishwa walirudi kwenye eneo hilo na wengine waliomba serikali ya kijiji kwa ajili ya kulima shamba hilo kwa muda.

Hata hivyo, Serikali ya kijiji cha Chamwino ilitoa sehemu ya eneo hilo kujengwa shule ya Sekondari ya Chanwino mwaka 1995 na sehemu ya shamba hilo lililotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Kikwete 2007.
Moja ya nyumba iliyopo eneo la mgogoro la Farm katika kijiji cha Chamwino Ikulu mkoani Dodoma ambapo ujenzi wake unaendelea

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na 4/1999 kifungu cha 13 (7) inaeleza kuwa ardhi iliyotengwa na halmashauri ya kijiji au mkutano wa kijiji kwa matumizi ya jumuiya/umma au ardhi ambayo wenyeji wa eneo husika wanaitumia kama ardhi ya kijiji ya umma kabla ya kutungwa kwa sheria ya ardhi, ardhi hiyo ni ya ardhi ya kijiji. Pia sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kifungu cha 12 (1) inakataza ardhi ya jumla kutolewa kwa mtu binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news