Serikali yafungua milango kwa Sekta Binafsi uzalishaji wa mbolea

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea hapa nchini ili kuhakikisha mbolea inapatikana kwa bei rafiki na kwa wakati.

Katika kutekeleza hilo tayari wawekezaji kadhaa wameshajitokeza kwa ajili ya kuwekeza hapa nchini. Miongoni mwa wawekezaji hao ni pamoja na umoja wa makampuni ya FEROSTAAL, HALDO TOPSOE na FAUJI ya Ujerumani ambao wameonesha nia ya kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea ya UREA kwa kutumia gesi.

Prof. Mkenda ameyasema hayo leo Oktoba 13, 2021 wakati akitoa hotuba kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo yalifanyika katika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani mwaka 2021 inasema “Tumia mbolea Bora kwa Tija na Kilimo Endelevu”.

"Kiwanda hiki kinatarajiwa kujengwa Mtwara na mazungumzo na Serikali yanaendelea. Aidha, mwekezaji Alhaji Dangote ameahidi kujenga kiwanda cha mbolea nchini ambapo mazungumzo yanaendelea na tayari a eneo la ujenzi wa kiwanda hicho mkoani Mtwara limeshapatikana,"amesema Waziri Prof.Mkenda.

Vilevile, Waziri Mkenda amesema kuwa, wawekezaji wa kampuni ya ITRACOM/FOMI kutoka Burundi wameshapatiwa eneo la kujenga kiwanda cha mbolea na ujenzi wa kiwanda hicho unaendelea jijini Dodoma.

Amesema, kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa samadi na madini ya phosphate na uzalishaji wake unakadiriwa kuwa tani 600,000 kwa mwaka.

"Aidha,Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, ameagiza kiwanda hiki kianze uzalishaji wa mbolea katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/23. Jitihada zote hizi za Serikali, zinalenga kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa bei nafuu na hivyo kuongeza matumizi ya viinilishe vya mimea (Plant nutrients) vitokanavyo na mbolea kutoka wastani wa kilo 19 hadi kilo 50 za virutubisho hivyo kwa hekta kama ilivyoazimiwa na wakuu wa nchi za Afrika kule Abuja mwaka 2007.

"Katika msimu wa kilimo (2021/2022) ulioanza mwezi huu wa Oktoba, 2021, tayari jumla ya tani 141,725.7 za mbolea zimeshaingizwa nchini na tani 117,900 ni bakaa ya mwaka 2020/21. Hii inafanya upatikanaji wa mbolea nchini kufikia jumla ya tani 283,625.7 za mbolea kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu wa kilimo,"amefafanua Waziri Prof.Mkenda.

Aidha, amesema kuwa, jumla ya tani 21,900 zinatarajiwa kuingizwa mwezi huu wa Oktoba, 2021 na kampuni za mbolea zinaendelea kuingiza mbolea.

Vilevile, amesema kiwanda cha Minjingu hadi kufikia mwezi huu wa Oktoba, 2021 kimezalisha jumla ya tani 4,050 na kinaendelea kuzalisha na kusambaza mbolea zake katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo mkoa huo wa Ruvuma ambapo alielezwa kuwa mbolea zao bei ya kiwandani ni shilingi 55,000.

"Serikali imeweka maafisa ugani katika kata na vijiji ili kutoa huduma za ugani kwa wakulima juu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

"Aidha, kuna vituo vya utafiti wa kilimo katika kila kanda. Nitoe wito kwa wakulima kutumia wataalamu hawa na kutumia matokeo ya tafiti wanayotoa ili tuweze kuzalisha kwa tija. Sambamba na hayo naendelea kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, maafisa ugani na watafiti kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo ikiwemo mbolea.

"Kwani mbolea inapotumiwa kwa usahihi sambamba na kilimo cha umwagiliaji, mbegu bora na viuatilifu bora ni dhahiri kuwa kutakuwa na uzalishaji mkubwa zaidi wa mazao ya chakula na kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda,"amefafanua Waziri Mkenda.

Prof. Mkenda amefafanua kuwa, ongezeko la uzalishaji wa mazao hususan mahindi ni matokeo ya matumizi ya pembejeo bora za kilimo ikiwemo mbolea.

"Hongereni sana wakulima nchini mkiwemo ninyi wa mkoa wa Ruvuma kwa uzalishaji mzuri. Mafanikio hayo, yamezalisha changamoto ya soko ambapo Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hiyo. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ni pamoja na kutoa zaidi ya sh.bilioni 100 kwa NFRA na CPB ili kununua mazao ya wakulima hasa mahindi ili kuwawezesha wakulima kupata fedha za kununua pembejeo kwa msimu huu,"ameongeza Waziri.

Mbali na hayo, Waziri Prof. Mkenda amesema kuwa, kutokana na upandaji wa bei ya mbolea katika soko la Dunia, Maafisa Ugani, Maafisa Kilimo,taasisi za utafiti na wadau wote wa kilimo wanapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima juu ya mbolea mbadala wa aina za mbolea walizozizoea.

Aidha, amesema wakulima waelimishwe namna ya kujitengenezea mbolea zao mbadala ambazo zitaendana na afya ya udongo katika maeneo yao.

"Ili kuwa na matumizi sahihi ya mbolea, ufahamu juu ya afya ya udongo ni muhimu, hivyo, niagize Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kutoa taarifa ya afya ya udongo kwa wakulima na wadau wengine ili kuhakikisha matumizi ya mbolea yaendane na mahitaji ya zao na udongo husika.

"Niwakumbushe wafanyabiashara kwamba Serikali imetoa fursa kwao kuagiza mbolea na kuiuza kwa wakulima kwa bei ya soko ili kumuwezesha mkulima kupata mbolea kwa wakati na kwa bei atakayoweza kuimudu. Kwa mantiki hiyo, hivi sasa ndio msimu wa kupanda na hivyo mbolea inahitajika kwa wingi mikoani, hivyo wafanyabiashara hakikisheni mnasambaza kwa wingi mbolea hizo mikoani ili ziwafikie wakulima kwa wakati,"amefafanua Waziri.

Pia Waziri Prof.Mkenda amewaomba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mbolea nchini ili kuchangia katika kuongeza upatikanaji na kupunga bei ya mbolea.

"Ni matumaini yangu kuwa maadhimisho haya yatakuwa chachu kwa wafanyabiashara wa mbolea kuendelea kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea bora, kwa bei nafuu na kwa wakati kwa ajili ya uhakika wa chakula na uchumi wa viwanda.

"Ninawashukuru tena waandaaji wa Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, washiriki wote wa maadhimisho haya pamoja na wadau wote waliotoa huduma mbalimbali zilizosaidia kufanikisha siku hii,"amesema.

Aidha, Waziri amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Prof. Anthony Manoni Mshandete kwa taarifa nzuri iliyochambua mafanikio makubwa katika ubora na biashara kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea na visaidizi vyake ikiwemo utengenezaji, uingizaji, utunzaji, usambazaji na uuzaji.

Amesema, taarifa hiyo inampatia faraja hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inaelekea kwenye njozi ya uchumi unaotegemea viwanda hasa ikizingatiwa kwamba viwanda vyetu nchini hutegemea malighafi zitokanazo na mazao ya kilimo kwa kiasi kikubwa.

"Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa kama alivyoeleza, ambazo wizara yangu itazichukua na kuzitafutia ufumbuzi. Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani hufanyika kila mwaka Oktoba 13 duniani kote. Maadhimisho haya ni kumbukizi ya uvumbuzi wa mbolea aina ya Amonia uliofanywa na Bw. Fritz Haber mwaka 1908 ambao ulichochea mapinduzi ya kijani katika karne ya 20 uliosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza janga la njaa katika nchi nyingi duniani,"amesema.

Mbali na Waziri ambaye alikuwa mgeni rasmi, maadhimisho hayo yaliwashirikisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo, Andrew Wilson Massawe, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Prof. Anthony Mshandete,Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma,Steven Mashauri Ndaki.

Wengine ni Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea,Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Eliuth Ngailo,Mrajis, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt.Benson Otieno Ndiege, wataalam wa kilimo kutoka Mkoa wa Ruvuma,Mkuu wa Wilaya ya Songea,Pololet Kamando Mgema, wakuu wa wilaya za Mbinga, Nyasa, Tunduru na Namtumbo.

Pia wengine ni wakurugenzi wa halmashauri za Madaba, Mbinga DC, Mbinga Mji, Nyasa, Nantumbo, Songea na Tunduru, wakuu wa idara na wataalam wa kilimo kutoka halmashauri za Songea,Mbinga, Nyasa, Nantumbo, Songea na Tunduru, wawakilishi wa vyuo vikuu,taasisi za utafiti na taasisi za kiraia, wazalishaji wa ndani wa mbolea na visaidizi vyake wakiwemo wafanyabiashara wa mbolea na visaidizi vyake.
Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda akisikiliza maelezo ya aina bora za mbolea kutoka kwa Bw. Michael Sanga ambaye ni Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo yamefanyika katika uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news