Serikali yaikabidhi SUMA JKT shamba la Bilioni 152/-

NA MWANDISHI MAALUM

Siku chache baada ya kununua shamba lenye ukubwa wa hekta 5,818 kutoka kwa mwekezaji aliyeshindwa kuliendesha na kulipa madeni ya mikopo, Serikali imelikabidhi shamba hilo kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) kwa lengo la kulisimamia wakati ikiangalia namna bora ya kuliendeleza. Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akipanda mti katika shamba la Mngeta kama ishara ya Serikali kukabidhi rasmi shamba hilo kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi Kujenga Taifa (SUMA-JKT) katika hafla ya makabidhiano ya shamba hilo lenye thamani ya sh, bilioni 152 lililopo Mngeta, Kilombero mkoani Morogoro.

Serikali ilinunua shamba hilo lililopo Mngeta, Kilombero mkoani Morogoro baada ya kushinda zabuni iliyoendeshwa na Mfilisi (Msimamizi wa Muda), Silvanus Mlola aliyewekwa na Benki ya NMB iliyokuwa inamdai mwekezaji, Kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL).

Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika shambani hapo, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto amesema shamba hilo linakadiriwa kuwa na mali zenye thamani ya Sh Bilioni 152 na hivyo kulifanya kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Ni dhahiri kuwa uwekezaji huu ni mkubwa na Serikali inahitaji kupata mapato kutoka uwekezaji huu thabiti na endelevu. Ni ukweli usiopingika kuwa wananchi wanaozunguka eneo hili watakuwa wanufaika wa kwanza wa mradi huu, na hivyo ni mategemeo ya Serikali kuwa SUMA JKT itafanya kazi kwa bidii katika kuendeleza mradi huu ili kutimiza lengo la Serikali. Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Brigedia Jenerali Absolomon Shausi wakipokea maelezo ya hali ya zana za kilimo zinazomilikiwa na Shamba la Mngeta wakati wa tukio la kutembelea na kukabidhiana rasmi ya shamba la Mngeta lililopo Kilombero, Morogoro kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali na (SUMA-JKT).

“Hatutegemei kuona shamba linadorora na kurudi kule tulipolitoa, zaidi tunatazamia muendelee kuboresha miundombinu na shamba lizalishe, muimarishe ulinzi kwenye mipaka inayozunguka shamba ili kuepusha uvamizi na migogoro ya ardhi na wananchi,” amesema Mgonya.

Baada ya makabidhiano hayo, Mgonya ameielekeza SUMA JKT kuandaa Mpango wa Biashara utakaoonesha nia na mikakati yao, ili uweze kuchambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Aidha, ili kulifanya shamba kujiendesha kwa tija, amesema baada ya uchambuzi wa mpango wa biashara na kubaini unafaa, Mamlaka inaweza kushauriwa kuundwa kwa kampuni tanzu chini ya SUMA JKT ambapo Serikali kupitia Msajili wa Hazina itakuwa na hisa kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa shamba hilo.

“Lengo ni kutaka kuona kwa pamoja tunafikia malengo na matarajio ya Serikali katika uwekezaji huu,” amesisitiza Mgonya. Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akipokea Mpango wa Mpito wa Matumizi ya Shamba la Mngeta kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Brigedia Jenerali Absolomon Shausi katika hafla ya makabidhiano rasmi ya shamba la Mngeta lililopo Kilombero, Morogoro. (Picha zote na Ofisi ya Msajili wa Hazina).

Akizungumzia wajibu na jukumu la Ofisi ya Msajili wa Hazina katika mradi huo, Mgonya amesema pamoja na majukumu mengine kama yalivyoanishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370, Ofisi ina jukumu la kuishauri Serikali na kusimamia uwekezaji wake katika Taasisi, Mashirika na Wakala za Serikali.

Na kwamba, katika mradi wa shamba la Mngeta, Ofisi yake inatekeleza moja ya matakwa ya Sheria, akisema walianza kwa kuishauri Serikali kulinunua shamba hilo na kupendekeza Shirika la SUMA JKT ambalo pia linasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina liwe mwendelezaji wa shamba la Kilombero.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Absolomon Shausi ameishukuru Serikali kwa hatua ya kulinunua na kuwakabidhi shamba hilo lenye manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo linalozunguka na Taifa kwa ujumla. Aidha, Brigedia Jenerali Shausi ameahidi kulisimamia na kuliendeleza shamba hilo ili kufikia malengo ya uwekezaji wa Serikali. Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT), Brigedia Jenerali Absolomon Shausi wakikagua shughuli za kilimo zinazoendelea katika shamba la Mngeta wakati wa tukio la kutembelea na kukabidhiana rasmi ya shamba hilo lililopo Kilombero, Morogoro kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali na SUMA-JKT .

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, aliyekuwa Mfilisi wa Shamba hilo, Mlola ameishukuru Serikali kwa ushirikiano na kukamilisha kwa wakati makubaliano yote yaliyofikiwa katika zabuni husika mpaka kufikia hatua ya mwisho ya makabidhiano na hivyo kuahidi kutoa ushirikiano wakati wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news