Serikali yatoa maelekezo kwa Shirika la Posta nchini

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

NAIBU Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Kundo Mathew amezindua duka la Posta Mtandaoni (Posta Online Shop) ambalo litawawezesha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kununua na kuuza bidhaa zao kwa njia ya mtandao huku akilitaka Shirika la Posta kujipanga kuteka soko la biashara mtandaoni kwani wana matawi 350 nchini.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa duka hilo ulioenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Posta Duniani, Naibu Waziri huyo amewaomba Watanzania kutumia huduma za shirika hilo kwani kwa sasa zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa.

Naibu Waziri huyo ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Ashatu Kijaji amesema shirika hilo ndilo lenye mtandao mkubwa hivyo wanatakiwa kujipanga kwani soko la biashara mtandao lipo mikononi mwao.

“Ndani ya nchi tuna matawi 350, hivyo kama watajipanga katika biashara ya mitandaoni soko lipo mikononi mwao tunatakiwa kuwa wabunifu kutoka na teknolojia tuliyonayo,” amesema.

Mathew amesema, uzinduzi wa duka hilo ni matokeo ya Maendeleo ya Teknolojia pia inakuja kutatua changamoto ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Amesema, duka hilo la posta mtandao litarahisishia wananchi waliopo maeneo ya pembezoni kupata huduma kwa haraka na kwa urahisi ambapo pia italeta tija na kuongeza kipato kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Dkt. Zainabu Chaula ameeleza kuwa kazi ya wizara ni kuweka miundombinu itakayoiwezesha nchi kwenda kwenye Tanzania ya kidigital na kuwaomba wananchi kutumia huduma za posta kwani ni salama.

“Nafurahi kuona tuna mafanikio umoja ni nguvu na ndio ambao utatuvusha kwani sisi tunatembea katika umoja,”amesema.

Naye, Kaimu Posta Masta Mkuu,Macrice Mbado amesema kutokana na badiliko makubwa ya Teknolojia ambayo yanaenda kwa kasi kubwa dunia shirika la posta limekuwa likifanya mageuzi na maboresho katika utoaji wa huduma zake ili kuendana na sera za Umoja wa mashirika ya posta duniani.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari,amesema sekta ya posta imepita katika changamoto nyingi ambapo amedai TCRA imetoa leseni 119 katika sekta ya Posta.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news